Hali ingali tete Somalia
20 Januari 2012 Mzozo wa Somalia haujamalizika kwani licha ya maendeleo madogo kupatikana mwaka uliopita, maisha ya watu 250,000 yangali hatarini. Hayo amesema, mratibu wa misaada ya kiutu ya Umoja wa Mataifa kwa Somalia, Mark Bowden. Akiomba msaada wa dola bilioni 1.5 kutoka kwa wafadhili wa kimataifa alisema:
"Hali bado ni tete nchini Somalia. Hadi watu milioni nne wanahitaji msaada wa aina moja au mwingine."
Sasa Umoja wa Mataifa ndio umetoa wito mpya kuomba msaada wa dharura ili kuzuia maafa zaidi. Umasikini mkubwa, mavuno mabaya na idadi kubwa ya mifugo inayokufa ni miongoni mwa mambo yanayozidisha matatizo ya watu hao katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Bei ya vyakula pia imeongezeka kwa asilimia 200 katika miaka iliyopita. Lakini vile vile kuna maendeleo kadhaa anasema, mratibu huyo wa misaada ya kiutu.
Kwa mfano, katika wilaya tatu, tatizo la njaa halipo tena. Watu wapatao milioni 2.6 wamepatiwa chakula: watu milioni 1.2 wanapata maji safi. Watoto milioni 1 wamechanjwa dhidi ya surua. Hiyo ni asilimia 51 ya umma uliolengwa kuchanjwa.
Hata hivyo, bado kuna matatizo makubwa anasema, Mark Bowden. Kwa maoni yake, ni lazima kuhakikisha usalama wa chakula. Mzozo wa chakula utaanza kupungua pale mavuno ya pili ya Somalia yatakapopatikana yaani katika miezi ya Agosti na Septemba. Tatizo jingine kuu ni hali ya wakimbizi anaeleza mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa, Mark Bowden.
"Mji mkuu Mogadishu unashughulikia wakimbizi wapya. Watu hao wapatao kama 185,000 wanategema misaada kutoka nje ili kuweza kuishi."
Lakini mashambulio yanayowalenga wafanyakazi wa mashirika ya misaada ni tatizo kubwa pia. Shirika la "Madktari wasio na mipaka" linaondoka kutoka maeneo ya mapigano mjini Mogadishu baada ya wafanyakazi wake wawili kuuawa. Hata chama cha kimataifa cha msalaba mwekundu kimesita kusafirisha chakula kusini mwa Somalia baada ya malori 140 kuzuiliwa na maafisa wa eneo hilo la kusini. Vile vile katika majuma ya hivi karibuni, mashambulio ya anga kutoka Kenya yameshika kasi katika eneo la Chuba kusini mwa Somalia.