1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali katika Mashariki ya Kati

13 Desemba 2004

Mgogoro wa Mashariki ya Kati umezua utata tena baada ya wanajeshi watano wa Israel kuuwawa katika shambulizi la bomu la hivi karibuni, tukio hili linatishia juhudi za kutafuta amani baada ya kifo cha Yasser Arafat. Wapiganaji wa kundi la Hamas wamejihusisha na shambulizi la bomu la hivi karibuni ambapo wanajeshi watano wa Israel wameuwawa.

Kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Palastina, Mahmud Abbas
Kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Palastina, Mahmud AbbasPicha: AP

Shambulizi hili ambalo lilipangwa kwa umakinifu lilitokea huko ukingo wa Gaza mpakani baina yake na Egypt wakati ambapo wapiganaji wa Kipalestina walilipua mabomu mawili kupitia upenyo wa chini kwa chini.

Israeli imejibu shambulizi hili kwa kulipua mji wa Gaza mapema leo, hadi kufikia sasa ripoti zinaashiria

kuuwawa kwa Wapalestina wawili lakini hakuna habari kuhusu majeruhi.

Shambulizi hili la bomu lenye uzito wa takriban kilo 1500 ni pigo kubwa kwa jeshi la Israel katika miezi saba iliyopita.

Israel imefunga mpaka baina ya mji wa Rafah na Egypt.

.Helicopter za Israel zililenga shabaha na kulipua karakana moja ya vyuma mjini Gaza kwa madai kuwa karakana hiyo ilitumika kutengeza silaha na shambulizi lingine likalenga Nyumba moja tupu karibu na chuo kikuu cha kiislamu.

Wadadisi wanaona kwamba mashambulizi haya yanatishia mazungumzo ya amani ambayo yalidhaniwa yangeleta kikomo cha uhasama wa vita vya miaka mingi baada ya kifo cha kiongozi wa Wapalestina Yasser Arafat. Wapiganaji wa Palestina kwa upande wao wanafanya mashambulizi kwa kile wanachokiona kuwa ishara ya ushindi kutokana na Israel kusisitiza mpango wake wa kuondoka kutoka ukanda wa Gaza, huku Israel nayo ikiapa kulipiza shambulizi lolote.

Waziri mdogo wa ulinzi wa Israel Ze’ev Boim kupitia kwa radio ya Israel ameuleza utawala wa Palestina juu ya kuzingatia amani ili Wapalestina wawe na uchaguzi wa urais wa amani unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Kujiuzulu kwa mwanasiasa mpinzani kutoka kwenye uchaguzi wa urais wa Palestina, umempa tumaini kubwa Mahamoud Abbas.

Marwan Barghouti mwanasiasa mpinzani aliyeko kizuizini alitangaza kujiuzulu kwake na hatiamae kumuunga mkono Mahmoud Abbas katika kukiwania kiti cha uongozi wa chama cha PLO kilichokaliwa hadi kifo chake na Yasser Arafat.

Nae Mahamoud Abbas ambae anashikilia uongozi hadi kupigwa kura, katika kuziba ufa wa kisiasa ulioachwa na kiongozi wa Wapalestina baiana ya Palestina na mataifa ya kiarabu aliomba msamaha kwa kile alichokitaja kwa Palestina kumuunga mkono Saddam Hussein wakati wa vita vya Ghuba vya mwaka tisini hadi tisini na moja.

Abbas atakuwa na kibarua kigumu cha kufanikisha mpango wa waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon wa kutaka kuihama Gaza. Mataifa ya ulaya yanaonelea kuwa hii itakua hatua muhimu kaatika kutafuta amani ya kudumu huko Mashariki ya Kati, huku wapalestina nao wakihofia gharama ya kupokwa ukingo wa magharibi wa mto Jordan.

Israel inasema iko tayari kufanya mazungumzo na viongozi wapya wa Palestina ikiwa wataacha siasa za vikundi vya kidini vyenye itikadi kali, vinginevyo Israel italazimika kukamilisha mpango wake wa kuondoka ukanda wa Gaza pekee, bila ushirikiano na Palestina

Zainab Aziz

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW