1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali kisiwani Madagascar

Oumilkher Hamidou17 Machi 2009

Jeshi lavamia kasri moja la rais huku rais Ravalomanana akijifungia katika kasri la pili kilomita zaidi ya 10 toka Antananarivo

Wanajeshi wanapiga doriaPicha: AP


Hali inasemekana ni shuwari katika maeneo ya karibu na kasri la rais mjini Antananarivo linalodhibitiwa na jeshi tangu jana.Wanajeshi kadhaa wanapiga doria karibu na kasri hilo.


Vifaru vitatu vilivyoshamiri mizinga, malori matatu ya kijeshi na dazeni kadhaa za wanajeshi waliovalia vikofia vyekundu wangali wanapiga doria mbele ya kasri la rais. Njia zote zinazoelekea kasri hilo la AMBOHITSOROHITRA zimefungwa na watu waliokusanyika kujionea yanayotokea wamerejeshwa nyuma na vikosi vya Gendarmerie. Wanajeshi wamewekwa ndani na nje ya kasri hilo.


"Hakukua na mapigano yoyote jana usiku na hali ni shuwari hivi sasa" amesema hayo afisa  mmoja wa kikosi cha kuingilia kati haraka kutoka kambi ya Ivato.


Umbali wa kilomita 12 kutoka mji mkuu Antananarivo, rais Marc Ravalomanana amejifungia katika kasri jengine la rais huko Iavoloha,akizungukwa na kikosi chake maalum na baadhi ya wafuasi wake.Anapinga kung'atuka, akihoji "atatetea haki yake hadi kufa."Walinzi wake na wafuasi wake wamezifunga njia zote zinazoelekea eneo hilo.


""Rais ameamua kusalia Madagascar,ameshawaambia walinzi wake waliomshauri akimbilie uhamishoni. "Amesema hayo msemaji wa ofisi ya rais Andry Ralijaona aliyekiri kwamba madaraka ya rais yamepungua; "Hii inaelekea kua njama ya mapinduzi ya kijeshi hii" Amesisitiza.


Licha ya hali hiyo inayotisha, wamalgash au wabuki kama wanavyojulikana wanajaribu kuishi maisha yao ya kawaida. Shule zimefunguliwa,sawa na maduka na baadhi ya wakaazi kadhaa wa mji mkuu wamekwenda kama kawaida makazini.


Umoja wa Afrika ambao mkutano wake ujao wa kilele ulikua ufanyike, kimsingi,  kisiwani Madagascar, umelaani "njama ya mapinduzi" na Umoja wa ulaya ukasema utasitisha misaada yake ikiwa kiongozi mpya ataingia madarakani kwa msaada wa nguvu za kijeshi.


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa jamhuri ya Tcheki, ambae ndie mwenyekiti wa sasa wa baraza la mawaziri la Umoja wa Ulaya, Karel Schwarzenberg, anasema:


"Umoja wa Ulaya unapinga, bila ya shaka, kitendo chochote cha matumizi ya nguvu na kama rais mpya atawekwa madarakani kwa msaada wa kijeshi, kinyume na katiba. Suala hilo tutalizingatia na tutafanya yale yale tuliyofanya mapinduzi yalipotokea Mauritania."


Kiongozi wa upinzani, meya wa zamani wa Antananarivo, Andry Rajoelina, ameunda serikali mbadala. Hata hivyo, anasema hajaliamuru jeshi lilivamie kasri la rais huko AMBOHITSOROPHITRA.


Mwandishi: Hamidou,Oummilkheir /AFP/Reuters

Mhariri: Miraji Othman







Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW