1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali mbaya ya hewa yasababisha watoto kupoteza makazi

6 Oktoba 2023

Majanga kutokana na hali mbaya ya hewa yalisababisha Watoto milioni 43.1 kupoteza makaazi yao kati ya mwaka 2016 hadi 2021.

Picha hii iliyopigwa Septemba 26, 2022 inayonyesha watoto walioondoka kwenye makazi yao kutokana na mafuriko wakinywa maji machafu nje ya makazi ya muda walikokuwa wakiishi, yaliyokuwa Jamshoro, jimbo la Sindh
Picha hii iliyopigwa Septemba 26, 2022 inayonyesha watoto walioondoka kwenye makazi yao kutokana na mafuriko wakinywa maji machafu nje ya makazi ya muda walikokuwa wakiishi, yaliyokuwa Jamshoro, jimbo la SindhPicha: Rizwan Tabassum/AFP/Getty Images

Hayo ni kulingana na ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Watoto UNICEF ambalo limesema majanga hayo yaliyochochewa na mabadiliko ya tabia nchi ni pamoja na mafuriko, ukame, vimbunga na moto wa misituni.

Kulingana na ripoti hiyo, mafuriko na vimbunga vilisababisha asilimia 95 ya makaazi yaliyopotezwa.

Laura Healy, mtafiti mwenza wa ripoti hiyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ilikadiriwa kuwa takriban Watoto 20,000 walilazimika kuyakimbia makaazi yao kila siku.

Hali hiyo inaonesha jinsi watoto walioathiriwa wako katika hatari ya kukumbwa na matatizo zaidi, kama vile kutengwa na wazazi wao au kuwa waathirika wa walanguzi wa watoto.

Wataalamu wametahadharisha kuwa katika miaka 30 ijayo, mafuriko yanaweza kusababisha watoto milioni 96 kuhama makaazi yao.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW