Hali mbaya ya hewa yatatiza safari ya chombo cha Spacex
28 Mei 2020Roketi kwa jina la SpaceX Falcon 9 lilitarajiwa kuanza safari kutoka Kituo cha Anga cha Kennedy majira ya saa 4:33 usiku kwa majira ya Marekani, kikiwabeba wanaanga Doug Hurley na Bon Behnken kwa safari ya masaa 19, wakiwa kwenye chombo chenye muundo mpya kiitwacho Crew Dragon kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga.
Kampuni ya SpaceXinayomilikiwa na bilionea Elon Musk nchini Marekani ndio iliyounda chombo hicho, na safari hiyo ingekuwa ya kwanza kufanyika na wanaanga wa Shirika la Anga za Juu la Marekani, NASA, kutokea kwenye ardhi ya nchi hiyo ndani ya kipindi cha miaka tisa.
Lakini dakika 17 tu kabla ya muda uliopangiwa chombo hicho kupaa angani, mratibu wa shughuli hiyo Mike Taylor alisema wamelazimika kuiahirisha, kwa sababu angani kulikuwepo hatari kubwa ya radi.
Trump alikuwepo tayari kushuhudia
Rais Donald Trump na Makamu wa Rais Mike Pence walikuwa tayari kituo chaNASA kwenye eneo la Cape Canaveral kushuhudia safari hiyo kwa macho yao.
Baadaye, Trump ambaye pia aliambatana na mke wake Melania, aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba atarejea Jumamosi, ilipohamishiwa ratiba mpya ya kukirusha chombo hicho angani.
Tangu mwaka 2011 Marekani imekuwa ikitegemea kituo cha Urusi kuwarushwa wanaanga wake wanaokwenda kwenye kituo cha kimataifa cha anga za mbali.
Ndoto ya NASA kwa muda mrefu
Safari hiyo ilikuwa imetajwa na mkuu wa NASA kuwa ni ndoto ya muda mrefu ya Marekani, yaani kurusha chombo cha Kimarekani, kutokea ardhi ya Marekani, kikiwa na wanaanga wa Kimarekani.
Ingawa shughuli hiyo imeahirishwa, kuhusika kwa kampuni ya Spacex kunamaanisha kwamba sasa NASA haiko peke yake kwenye soko la masuala ya anga za juu, jambo ambalo mkuu wa shirika hilo, Jim Bridenstine, anasema kuwa ulikuwa uamuzi mgumu sana kuufikia.
Kwa utaratibu rasmi, safari kuelekea Kituo cha Kimataifa cha Anga ni ya majaribio. Inahusu kuonesha kwamba chombo hicho kinafanya kazi, kwamba mchakato uko sahihi, na kwamba mifumo inakwendana.
(afpe,ape, rtre)