1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Somalia baada ya rais kutaka kumng'oa madarakani waziri mkuu

Oumilkher Hamidou15 Desemba 2008

Bunge la Somalia lamuunga mkono kwa wingi mkubwa waziri mkuu na serikali yake

Ramani ya SomaliaPicha: AP Graphics/DW


       Bunge la Somalia limeamua kumuunga mkono waziri mkuu na serikali ya mpito dhidi ya rais Abdullahi Yusuf Ahmed aliyetangaza kulivunja baraza la mawaziri na kwa namna hiyo kuzidi kuididimiza nchi hiyo ya pembe ya Afrika katika janga la kisiasa linalokorofisha juhudi za amani.


Siku moja tuu baada ya rais Abdullahi Yusuf Ahmed kusema ameamua kumng'oa madarakani waziri mkuu Nur Hassan Hussein na kuivunja serikali yake,bunge la mpito,likikutana kwa kikao maalum huko Baidoa,umbali wa kilomita 250 kaskazini magharibi ya mji mkuu Mogadishu,limemuacha mkono rais na badala yake kumuunga mkono kwa nguvu waziri mkuu.


"Wabunge 143 wanaitambua serikali,20 wamepinga na sabaa hawajapiga kura upande wowote" amesema hayo spika wa bunge Aden Mohammed Nur,baada ya kura kuhesabiwa hii leo katika kikako hicho maalum.


"Kwa hivyo,serikali ya Nur Hassan Hussein ni halali"-ameongeza kusema spika huyo.


Jana rais wa Somalia  Abdullahi Yusuf Ahmed alitangaza kuivunja serikali na kumtoa madarakani waziri mkuu akihoji "wameshindwa kutekeleza jukumu lao."


"Nnalazimika kuinusuru nchi"-amesema rais huyo.

"Rais amejisemea mwenyewe,bila ya kuzingatia kanuni na sheria.Hana haki ya kumpokonya madaraka waziri mkuu wa serikali kuu ya mpito" alijibu hapo hapo waziri mkuu Nur Hassan Hussein kupitia shirika la habari la ufaransa AFP.


Kwa mujibu wa muongozo wa serikali kuu ya muungano,rais hawezi kumpokonya wadhifa wake waziri mkuu,bila ya idhini ya bunge.


Bwana Yusuf anasema ataheshimu uamuzi wa wabunge..


Shughuli za taasisi za mpito zimepooza tangu wiki kadhaa sasa kutokana na mivutano kati ya rais na waziri mkuu,katika wakati ambapo waasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam wanazidi kusonga mbele huku mazungumzo ya amani yakizorota.


Viongozi hao wawili wanashindana pia kuhusu namna ya kukabiliana na wapinzani wa kiislam.


Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Jean Ping amesema hii leo ameingiwa na wasi wasi kutokana na uamuzi wa rais wa Somalia.


"Uamuzio huo utazidi kukorofisha mambo,utazidisha mfarakano katika serikali kuu ya mpito na unatishia kuvuruga juhudi za kimataifa za kumalaiza vita vya wenyewe kwa wenyewe."Mwisho wa kumnukuu  Jean Ping.


Umoja wa Afrika uliotuma kikosi cha kulinda amani mjini Mogadischu-AMISOM-kilichogeuka shabaha ya hujuma za waasi wa kiislam,unashauri vikosi vya Umoja wa mataifa viwekwe nchini humo.


Ethiopia iliyotuma wanajeshi wake nchini Somalia mwishoni mwa mwaka 2006,imetangaza kuwarejesha nyumbani wanajeshi hao mapema mwakani.





Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW