Hali ngumu ya kusubiri kwa Merkel katika uchaguzi wa Hesse
28 Oktoba 2018Serikali kuu iliyoko katika mji mkuu Berlin imeshusha pumzi tangu pale wakaazi wa jimbo la Bavaria walipouwaadhibu washirika wa Merkel , chama cha kihafidhina cha Christian Social Union CSU na kile cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Social Democratic SDP, katika uchaguzi wa jimbo mapema mwezi huu.
Kikilenga kupuuzia vita vya ndani ambavyo vimesababisha kuwakimbiza wapiga kura kutoka vyama vikuu vitatu vya asili, viongozi wametoa wito wa kuwa na nidhamu na bila kufukuzana kabla ya uchaguzi kuanza mapema leo, ambapo watu milioni 4.4 wana haki ya kupiga kura katika jimbo la Hesse, ikiwa ni asilimia saba tu ya wapiga kura nchi nzima.
"Je Hesse itaripua serikali ya inayojulikana kama "ushirika mkuu"? mjini Berlin kati ya chama cha kansela Merkel cha Christian Democratic Union CDU na kile cha SPD , gazeti linalouzwa zaidi nchini Ujerumani la Bild limeuliza.
"Hesse yapiga kura , Berlin yatetemeka," limeandika gazeti la Sueddeutsche Zeitung.
"Kansela hajawahi kuwa katika mbinyo mkubwa kama huu."
Matokeo mabaya
Matokeo mabaya kwa ama CDU ama SPD yatafungua duru mpya ya kuelekezana vidole na miito ya kuachana na "ushirika mkuu" wa tatu wa kansela huyo wa muda mrefu usio na mapenzi ya kweli."
Wengi katika jimbo la Hesse kwa kiasi kikubwa wanaridhika na serikali yao ya jimbo, ikiwa na maana "hakutakuwa na hali inayoelekeza mabadiliko miongoni mwa wapiga kura wa Hesse bila nia ya kutuma ujumbe mjini Berlin," gazeti la kila wiki la Die Welt am Sonntag limeeleza katika maoni yake.
Ishara ya kwanza ya kuporomoka kwa Merkel itakuja saa 12 jioni saa za Ulaya ya kati wakati vituo vya kupigia kura vitakapofungwa na matokeo ya kwanza kuonekana.
Uchunguzi unaelekeza kwa waziri mkuu wa jimbo hilo kutoka CDU na mfuasi mtiifu wa Merkel Volker Bouffier na mpinzani wake kutoka chama cha SPD Thorsten Schaefer-Guembel wakipata vipigo vikubwa ikilinganishwa na mwaka 2013.
Vyama vyote viwili vinatarajiwa kupoteza kiasi ya alama 10, katika matokeo ambayo CDU inaweza kupata juu ya 20 na karibu na 20 asilimia kwa SPD.
Kutegemea vipi vyama hivyo vitaweza kufanya katika uchaguzi huo, hesabu za vyama hivyo shirika katika serikali kuu zinaweza kuruhusu ama kuongoza serikali mpya ya jimbo, na kuwapa Merkel ama kiongozi wa SPD Andrea Nahles ushindi wa kiishara.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
mhariri: Grace Patricia Kabogo