Hali ngumu ya maisha katika Zimbabwe inazidi kuleta wasiwasi.
1 Agosti 2007Jana Benki Kuu ya nchi hiyo ilitoa noti mpya ya juu kabisa ambayo ni mara mbili ya thamani ya ile ya hapo kabla. Ilitajwa kwamba kusambazwa kuanzia leo kwa noti hiyo ya dola laki mbili za Zimbabwe kutarahisisha shughuli za kibiashara.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, limesema mamilioni ya wananchi wa Zimbabwe watategemea misaada ya kiutu ifikapo mwisho wa mwaka huu. Lilimewaomba wafadhili wasaidie katika operesheni ya kutoa misaada ya vyakula nchini humo itakayogharimu dola milioni 118. Shirika hilo lilisema linapanga kuwalisha mnamo miezi minane ijayo mara kumi idadi ya watu wanaofaidika na mpango kama huo hivi sasa ili kuepusha kutokea kitisho ya njaa kubwa. Ili kufanya hivyo, Bwana Amir Abdulla, mkurugenzi wa WFP kwa eneo la Kusini mwa Afrika, alisema wanahitaji misaada zaidi, tena kwa haraka. Shirika hilo linalowasaidia watu laki tatu huko Zimbabwe kila mwezi, lilisema bila ya kupata fedha zaidi akiba yake ya vyakula itapungua ifikapo Septemba na kutobakia chochote mwishoni mwa mwaka. Makundi mengine ya misaada yanayosaidiwa na Marekani yanawalisha watu wengine laki nane. Mavuno yajayo ya Zimbabwe yaanatarajiwa April mwakani.
Hivi sasa Zimbabwe ina matatizo makubwa ya kiuchumi, na wahakiki wanamlaumu rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe, kutokana na siasa zake za ubishi.
Pia hivi sasa nchi hiyo inajionea ughali mkubwa kabisa wa maisha na mfumko wa haraka kabisa wa bei za bidhaa kuonekana duniani. Kuna upungufu mkubwa wa vyakula na mafuta na ukosefu mkubwa wa nafasi za kazi katika nchi ambayo hapo zamani ilikuwa inailisha Kusini mwa Afrika. Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, lilikisia jana kwamba ughali wa maisha katika Zimbabwe ifikapo mwaka huu utapanda kwa asilimia laki moja.
Mohammed Dedes huko Visiwani Zanzibar anaihofia hali hiyo ya Zimbabae:
Noti mpya ya dola za Ki-Zimbabwe laki mbili ina thamani ya dola 13 za Kimarekani katika mabadilishano kwa rasmi ya sarafu, lakini katika masoko ya magendo ni sawa na dola moja tu ya Kimarekani. Benki ya Zimbabwe jana haijataja juu ya ughali mkubwa wa maisha katika nchi hiyo ambao umepelekea mirundo mikubwa ya manoti kuhitajika ili kununulia vitu vya kawaida madukani. Kwa hakika manoti hayo sasa yamekuwa hayana faida kabisa katika nchi hiyo.
Tena Mohammed Dedes, mwanauchumi wa Visiwani Zanzibar…
Kampeni, ilioongozwa na serekali hivi karibuni ya kulazimisha bei za bidhaa zipunguzwe kwa zaidi ya nusu, zimefanya maduka yasiwe na bidhaa kwenye mashubaka, kwa vile wafanya biashara hawamudu kununua bidhaa mpya.Lakini rais Mugabe amebakia kuwa mkakamavu, licha ya kuwekewa mbinyo aumalize mzozo huo. Amekuwa akiukandamiza upinzani na kuyatuhumu madola ya Magharibi kwamba yanafanya njama ya kutaka kumpinduwa kutoka madarakani na kuuendea kichini chini uchumi wa Zimbabwe kwa kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Shirika la Mipango ya Chakula Duniani limesema bila ya kutolewa misaada, familia zisizojiweza zitalazimika kuchukuwa hatua za hatari za kulinda uhai wao, labda kula vyakula vya sumu vinavopatikana mwituni, kuuza vitu vyao vya majumbani walivobakia navyo, kujiuza kimwili ili wapate vyakula na kuuvuka mpaka kwa njia haramu ili kuingia Afrika Kusini.
Na licha ya kwamba mabwawa yamejaa maji kwa zaidi ya asilimia 60, mifereji katika mji mkuu wa Harare haitoi maji. Zaidi ya nusu ya wakaazi milioni tatu wa Harare wana shida ya kupata maji. Watu wengine hubeba madebe ya maji wanapokwenda makazini. Pia mataka majiani yamesheheni, hata wazee wengine wanawakataza watoto wao kucheza nje ili wasiambukizwe na magonjwa.