Hali ni tete Libya
25 Februari 2011Wanajeshi wanaomuunga mkono Kanali Muammar Gaddafi,waliojihami kwa silaha nzito wanaripotiwa kuendelea na harakati za kujaribu kuwazuwia waandamanaji katika miji ya eneo la magharibi iliyo karibu na mji mkuu wa Tripoli.Hata hivyo eneo la mashariki ya Libya limetekwa na waandamanaji wanaompinga Kanali Muammar Gaddafi.Wakati huo huo waandamanaji wanajiandaa kufanya maandamano makubwa zaidi hii leo.
Az-Zawia kwatokota
Watu 23 wanaripotiwa kuwa wameuawa na wengine 44 wamejeruhiwa katika mji wa Az-Zawia ulio eneo la magharibi mwa mji wa Tripoli.Mauaji hayo yalitokea hapo jana pale wafuasi wa uongozi wa Libya walipopambana kwa ghadhabu na waandamanaji wanaoipinga serikali katika mji huo ulio na umuhimu mkubwa katika sekta ya mafuta.Kulingana na taarifa za gazeti moja ambalo kwa sasa limehamishia operesheni zake katika eneo la mashariki,majeruhi wanashindwa kufika hospitalini kwa sababu milio ya risasi inasikika kila mahali.
Mipaka yafurika
Mapigano makali pia yanaripotiwa kutokea katika mji wa tatu kwa ukubwa wa Misrata.Hali ni ya wasiwasi katika eneo la Zouara lililo karibu na mpaka wa Libya na Tunisia.Wafanyakazi wa Kimisri wanaripotiwa kulikimbilia eneo la mpakani kwani mji huo kwa sasa umetekwa nyara na wapiganaji wa kiraia.
Akilihutubia taifa hapo jana,Kanali Muammar Gaddafi aliwalaumu wakazi wa mji wa Az-Zawia kwa kumuunga mkono kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda,Osama bin Laden.
Kiongozi huyo wa Libya alilihutubia taifa hilo lililogawika kwa simu tofauti na alivyofanya mwanzoni mwa wiki hii alipoonekana moja kwa moja kwenye kituo cha taifa cha televisheni.Hali hiyo inaashiria kuwa huenda udhibiti wake umepungua na hajulikani aliko hasa.
Mkono wa Al-Qaeda?
Kwa upande wake,tawi la eneo la kaskazini mwa bara la Afrika la kundi la Al-Qaeda limeahidi kuwa litafanya kila liwezalo kuwasaidia wanaoupinga uongozi wa Libya.Hayo ni kwa mujibu wa taarifa yao iliyochapishwa kwenye mtandao wa kundi hilo la AQIM.
Barabara za mji wa Tripoli zinaripotiwa kuwa tupu ila hii leo watu wanatazamiwa kuenda misikitini kwa sala ya adhuhuri.
Kulingana na mwandishi wa shirika la habari la AFP,kwa sasa mji wa Benghazi unadhibitiwa na wapinzani wa Kanali Gaddafi.
Baadhi ya waandamanaji walizitundika sanamu za kiongozi wao,Muammar Gaddafi,kwenye milingoti ya taa za barabarani.Vituo vya polisi vimetiwa moto ila hakuna wizi wowote ulioripotiwa kutokea.
Mahakama yateketezwa
Kwengineko,wapinzani wa serikali waliunda makao makuu mapya katika mahakama kulikoanzia maandamano hayo.Wanajeshi kadhaa nao wanaripotiwa kuziuza silaha zao ijapokuwa makamanda wao wako katika harakati za kuwakusanya kwa minajili ya kumuunga mkono kiongozi wa Libya.
Serikali ya Libya inajaribu kuwarai raia wake na hii leo itawasambazia vitita vya pesa zitakazotumiwa kugharamia bidhaa za matumizi.Kulingana na tangazo la kituo cha televisheni cha taifa,kila familia itapokea kiasi ya dola 400 zitakazotumiwa kufidia gharama za maisha zilizoongezeka nao wafanyakazi wa sekta ya umma wataongezewa mishahara kwa asilimia 150.
Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/RTRE/DPAE
Mhariri:Josephat Charo