1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali shwari N'djamena kabla ya mazishi ya rais Idriss Deby

Saleh Mwanamilongo
22 Aprili 2021

Hali ni shwari N'djamena siku tatu baada ya kutangazwa kifo cha Idriss Deby,huku upinzani ukipaza sauti kutaka kuweko na uongozi wa kiraia nchini humo.

Hali jijini N'djamena mji Mkuu wa Chad,Jumatano April 21,2021 siku mbili baada ya kifo cha rais Idriss Deby.
Hali jijini N'djamena mji Mkuu wa Chad,Jumatano April 21,2021 siku mbili baada ya kifo cha rais Idriss Deby.Picha: Djimet Wiche/AFP

Mji Mkuu wa N'djamena ulionekana kuwa tulivu asubuhi ya leo Alhamisi. Mwandishi habari wa DW alishuhudia baadhi ya vifaru vya kijeshi kwenye baadhi ya maeneo ya mji na kwenye Ikulu. Masoko yalifungua na hata baadhi ya ofisi za umma zilifanya kazi. Umoja wa Afrika,umoja wa Ulaya na hata Umoja wa Mataifa bado kutoa msimamo wa wazi kuhusu hali inayoendelea nchini Chad.

Mazishi ya rais Idriss Deby yanatarajiwa kufanyika kesho Ijumaa kwenye mji Mkuu wa Chad, Ndjamena. Rais wa Ufaransa Emamanuel Macron na Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrel wamesema watahudhuria mazishi hayo. Waasi wanaojulikana kama "Front for Change and Concord", wamewatahadharisha marais wa kigeni kutohudhuria mazishi hayo na wametaka uwepo uongozi wa kiraia.

Waasi hao wamesema hawautambuwi utawala wakijeshi,uliochukua madaraka nchini Chad. Upinzani na asasi za kiraia pia zimetoa mwito wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya kuwezesha kuwekwa serikali ya mpito ya kiraia.

''Mtoto sio baba yake''

Jenerali mahamat Idriss Déby,mtoto wa Deby na kiongozi wa kijeshi nchini Chad,ambayeamechukuwa nafasi ya babake.Picha: Presidency of the Republic of Chad

Antoine Glaser,mtaalamu wa Chad amesema uteuzi wa Mahamat Idriss Déby, kuongoza Baraza la Mpito la Kijeshi,umeiingiza nchi hiyo katika hali ya sintofahamu, kwa sababu Mahamat hana ushawishi kama wa babake.

''Mtoto sio baba yake, Deby alichukuwa madaraka wakati akiwa na ushawishi wa eneo alikotokea na katika jeshi. Lakini huyu mtoto wake anakabiliwa na upinzani mkali wa makundi ya waasi na hata ndani ya jeshi. Kwa hiyo ni vigumu kutabiri kitakacho tokea'', alisema Glaser.

Hali ya wasiwasi ilitanda mapema hapo jana Jumatano juu ya umbali wa kiasi gani waasi watakuwa wameukaribia mji mkuu wa N'Djamena, ulio na idadi ya watu milioni 1, na iwapo jeshi lingeendelea kuwa tiifu kwa Mahamat Deby baada ya kifo cha baba yake aliyedumu madarakani kwa miongo mitatu.

Maombolezo ya kifo cha Deby

Taarifa za ujio wa waasi hao zimezua hofu katika mji wa N'Djamena, ambao uliwahi kushambuliwa na kundi jingine la waasi mnamo mwaka 2008. Maafisa wa baraza la kijeshi wamesema mapambano ya kuwania udhibiti wa nchi bado hajakwisha.

 Nchi za Sahel, mfano wa Mali,zimetangaza  siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha rais Deby. Rais wa Congo, Felix Tshisekedi ambaye pia ni mwenye kiti wa sasa wa Umoja wa Afrika alitangaza pia kesho Ijumaa kama siku ya maombolezo ya kitaifa nchini mwake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW