Hali tete Ufaransa watu 150 wakamatwa usiku kucha
29 Juni 2023Mapambano kati ya polisi na waandamanaji na ghasia za kuchoma moto magari, na vitu vingine zilitokea kwenye kitongoji cha Nanterre na kwenye maeneo mengine ya magharibi ya mwa mji wa Paris. Ghasia hizo pia zimeenea katika miji mingine. Kutokana na hali hiyo ya machafuko maalfu ya polisi wamepelekwa ili kuzizima ghasia hizo. Wizara ya mambo ya ndani imesema polisi 2,000 wamepelekwa kukabiliana na hali ya mjini Paris na miongoni mwao kadhaa wamejeruhiwa baada ya mapambano na waandamanaji waliokuwa na ghadhabu.
Mauaji ya Nahel kwenye ukaguzi wa trafiki yaliyonaswa kwenye video, yaliishtua nchi na kuchochea mvutano wa muda mrefu kati ya polisi na vijana wanaoishi kwenye makazi yaliyo katika vitongoji vya watu wenye maisha duni.
Waandamanaji wenye hasira walichoma moto magari, mapipa ya takataka na majengo ya umma katika vitongoji vya Paris na machafuko yakaenea katika miji mingine ya Ufaransa licha ya kuongezwa idadi wa walinda usalama na wito wa rais Macron wa kuwataka watu wawe watulivu.
Kabla ya kuanza mkutano na mawaziri wake rais wa Ufaransa Emannuel Macron alisema ni wazi hisia zilizopo baada ya kifo cha kijana huyo zinahitaji kutafakari lakini amesema hilo litaweuekana tu utulivu utadumishwa. Amesema na hicho ndicho serikaliyake inakihimiza mara kwa mara.Macron amesema matukio ya vurugu dhidi ya vituo vya polisi, shule, kumbi na taasisi za Jamhuri hayana uhalali kabisa.
Video ya shahidi mmoja aliyorekpdi tukio hilo kwa kutumia simu yake, na ambayo imethibitishwa na mtandao wa mawsiliano wa Ufaransa, Info channel, inamwonyesha afisa wa polisi akielekeza bunduki yake kwa dereva wa gari ambalo lilikuwa limesimama. Wakati kijana huyo ghafla alipoendesha gari lake, afisa huyo alimfyatulia risasi na kumjeruhi vibaya.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Gérald Darmanin ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba usiku huo ulitawaliwa na vurugu zisizoweza kuvumilika ambapo maeneo ya umma kama kumbi, shule na vituo vya polisi vilichomwa moto au kushambuliwa.
Afisa aliyehusika katika kadhia hiyo yuko chini ya ulinzi wa polisi na amachunguzwa kwa tuhuma za kuua bila kukusudia. Leo hii Alhamisi, maandamano kuelekea kwenye mazishi yamepangwa katika kitongoji cha Nanterre kwa ajili ya kutoa heshima na kumbukumbu ya kijana huyo aliyeuawa.
Vyanzo:DPA/RTRE