1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya afya ya Clinton yatia mashaka

14 Septemba 2016

Hali ya afya ya mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi nchini Marekani Hillary Clinton, hatua ya kusitisha mapigano nchini Syria na mapambano dhidi ya ugaidi nchini Ujerumani

Hillary Clinton mit Handy
Hillary Clinton mgombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi nchini MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Drew

hayo ndio yaliyoandikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo Jumatano(14.09.2016).

Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger likiandika kuhusu hali ya afya ya mgombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa Marekani, Hillary Clinton, mhariri anaandika kwamba iwapo taifa hilo lingefahamu kuhusiana na hali ya afya ya Franklin D. Roosevelt ama John F. Kennedy, isingekuwa rahisi kwa yeyote kati ya hao kuwa marais katika nchi hiyo.

Pamoja na hayo lakini kuhusiana na uwezo wa kuongoza, hali ya afya haina umuhimu sana. Katika uchaguzi huu kuna hali ya kufadhaisha hata hivyo. Suala hilo linaelekea kupandisha joto la wasi wasi. Maambukizi ya mapafu aliyopata Clinton, yanakwenda mbali zaidi. Ni kuhusu madaraka makubwa ya nchi hiyo, na suala la vipi na wapi utaratibu wa dunia unaelekea katika miaka ijayo. Kwa wakati huu mtu atajiuliza, Marekani kweli itaendelea kuwa taifa kubwa lenye madaraka duniani?

Gazeti la Der neue Tag kuhusu mada hiyo limeandika kwamba, Clinton kuficha kuhusu ugonjwa wake ni kosa la pili katika muda wa hivi karibuni kabisa baada ya kuwatusi wafuasi wa Trump kuwa ni wabaguzi bila kiasi na wabaguzi wa kijinsia . Kukaa kimya kwa Trump kuhusiana na haki ya kujua kuhusu hali ya kiafya ya wagombea ina sababu yake. Bilionea huyo anaichukulia hali ya marejesho ya mahesabu ya matumizi yake , kuwa kama siri kubwa ya kitaifa. Kwa kiasi kikubwa hali hiyo itamharibia zaidi kuliko ilivyo kwa mpizani wake.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de Mistura akiwasili kwa ajili ya mkutano na waandishi habari GenevaPicha: picture-alliance/Xinhua/X. Jinquan

Katika mada ya usitishaji mapigano nchini Syria mhariri wa gazeti la Stuttgarter Nachrichten linaandika kwamba hali halisi katika mashariki ya kati ni kwamba hali ni mbaya , kuliko serikali nyingi za mataifa ya magharibi yaliyofikiria katika muda wa miaka mitano iliyopita, kwamba kuondolewa madarakani kwa rais Bashar al-Assad ni suala la wiki kadhaa tu. Tathmini hii potovu inaelekeza katika matatizo mawili.

Makundi ya wenye itikadi kali yenye silaha kwa muda mrefu yamepewa msaada wa fedha na hata silaha, baadhi hayana mafunzo ya kutosha. hali hii ya kutokuwa na uwazi inafanywa na Uturuki, ambayo wazi kabisa inalisaidia kundi la IS na haikosolewi.

Mataifa ya magharibi yanayoshirikiana katika vita hivi, Nani atasaka amani na kuitekeleza? Anauliza mhariri.

Kwa hiyo hali itabakia hivyo hivyo, kama ilivyokuwa mwaka 2010, watu wataendelea kuuwawa , hadi Syria itakapokuwa tena chini ya udhibiti wa dikteta Bashar al-Assad.

Kuhusu suala la mapambano dhidi ya ugaidi nchini Ujerumani, mhariri wa gazeti la Lübecker Nachrichten anaandika , kwamba mjadala mkali kuhusiana na sera juu ya wakimbizi unapata msukumo mpya.

Usiku katika mji wa Reinfeld unamsukua kila kitu katika mjadala huo , hususan majibu rahisi kuhusu suala hilo. Hali hii inazuwia uwezo wa kutoa maelezo. Hili ni suala la kila mtu anayeamini kuhusu demokrasia, ambapo watu wenye busara wanapaswa kujitokeza kutoa mawazo yao. Watu waendelee kuwa macho na sio kusubiri hadi panapotokea shambulio. Watu wanatakiwa kuona hatari na kuchukua hatua haraka. Hii ni hatua ya kulinda uhuru na sio kuwa wahanga na kuwa na woga.

Mwandishi: Sekione Kitojo/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Khelef