1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya Bazoum yaitia wasiwasi Jumuiya ya Kimataifa

11 Agosti 2023

Ripoti zinasema rais Bazoum anayezuiliwa na jeshi lililofanya mapinduzi amekaa bila chakula,umeme wala huduma za afya kwa siku chungunzima,Umoja wa Afrika wasema hatua hiyo haikubaliki

Rais  Macron na Mohamed Bazoum
Rais Mohamed Bazoum akisalimiana na mwenyeji wake wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyemtembelea Paris Februari mwaka huuPicha: Michel Euler/AP/picture alliance

Khofu kuhusu kuendelea kushikiliwa na jeshi kwa rais Mohamed Bazoum nchini Niger inaongezeka. Jumuiya ya kimataifa ina wasiwasi na hali ya rais huyo aliyepinduliwa madarakani na jeshi.

Baada ya Jumuiya ya ECOWAS kuidhinisha kupeleka kikosi cha dharura nchini Niger kurudisha utawala wa kikatiba, wakuu wa majeshi wa nchi za Jumuiya hiyo imeelezwa kwamba watakutana wiki ijayo katika mji mkuu wa Ghana,Accra kwa mazungumzo kwa mujibu wa msemaji wa ECOWAS.

Viongozi wa ECOWAS waliokutana Alhamisi Abuja kuhusu NigerPicha: Gbemiga Olamikan/AP/picture alliance

Hivi sasa lakini khofu imeongezeka juu ya hali ya rais aliyepinduliwa Mohammed Bazoum. Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wameungana na Marekani na nchi nyingine kutowa tahadhari juu ya hali ya kiongozi huyo aliyechaguliwa kidemokrasia nchini Niger.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Joseph Borrell akinukuu ripoti alizonazo hivi sasa amesema Bazoum na familia yake hawana chakula,umeme wala huduma ya matibabu kwa siku kadhaa,na akatowa mwito wa kurudishwa mara moja madarakani kiongozi huyo.

Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Umoja wa Afrika

Umoja wa Afrika pamoja na kuzungumzia wasiwasi wake juu ya hali ya rais Bazoum pia imeahidi kuiunga mkono Jumuiya ya ECOWAS huku mwenyekiti wa tume ya Umoja huo wa Afrika Moussa Faki Mahamat akisema anaunga mkono uamuzi wa jumuiya hiyo kueleka mapinduzi ya Niger.Moussa Faki amesema mazingira anayoshikiliwa rais Bazoum yanatia wasiwasi.

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa, Bazoum anazuliwa katika makaazi ya rais yeye na familia yake na maafisa wengine.

Duru ya karibu na Bazoum imeeleza kwamba yuko katika hali ya kawaida,japo mazingira aliyopo ni magumu na kwamba viongozi wa kijeshi wameendelea kutowa kitisho cha kumdhuru ikiwa itatokea jeshi kuivamia Niger.Rais wa Ivory Coast Alassane Outtara jana alisema wanajeshi wa Niger wanamshikilia mateka rais Bazoum na kitendo hicho ni ugaidi.Soma pia: ECOWAS yaidhinisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Niger

Katika mkutano wa kilele uliofanyika jana Abuja huko Nigeria ECOWAS iliwaagiza wakuu wa majeshi wa jumuiya hiyo kuandaa kikosi cha dharura kitakachoweza kupelekwa Niger ingawa pia Jumuiya hiyo ikasisitika kwamba kipaumbele chao kikubwa ni kuendelea na njia za kidiplomasia.

Afisa wa jeshi la Niger akisalimiana na ujumbe wa kijeshi wa Burkina Faso katika uwanja wa ndege wa NiameyPicha: RTN/Reuters

Washirika wa Niger

Mali na Burkina Faso zote zikiwa zinaongozwa na tawala za kijeshi zimetahadharisha juu ya kuingiliwa kijeshi Niger kwa kusema kwamba hatua hiyo itakuwa inatangaza vita dhidi ya mataifa yao.

Mali, BurkinaFaso pamoja na Guinea na Niger yenyewe hazikushiriki mkutano wa Abuja. Na wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema jeshi la ECOWAS  huenda likachukuwa wiki kadhaa au hata zaidi kukusanywa na hadi wakati huo ipo nafasi ya mazungumzo.

Ivory Coast ni nchi pekee ambayo mpaka sasa imeshasema itatuma kikosi cha wanajeshi 850. Benin imesema itachangia wanajeshi lakini haikutaja wangapi wakati nchi nyingine nyingi ikiwemo Nigeria inayoshikilia uwenyekiti wa ECOWAS  zikiwa mpaka sasa bado hazitaki kusema idadi ya askari itakaochangia.Gambia na Liberia zimesema leo kwamba bado hazijaamua kuhusu kutoa wanajeshi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW