1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya COVID 19 ikoje mpakani mwa Burundi na Tanzania?

1 Machi 2021

Licha Serikali ya Burundi kufunga mipaka yake ya majini na nchi kavu tangu Januari 11 kwa ajili ya kujihadhari na virusi vya Corona, raia wa maeneo hayo wanaendelea na shughuli zao bila kuchukua tahadhari za kujikinga.

Tansania Dar es Salaam Coronavirus
Picha: DW/E. Boniphace

Idhaa ya Kiswahili ya DW imeshuhudia hali hiyo katika eneo la Mwibambo, Wilaya ya Giteranyi mkoa wa Muyinga nchini Burundi mpakani mwa Tanzania na Burundi liliko Soko maarufu la Mwibambo, lenye muingiliano mkubwa wa watu kutoka nchi zote mbili

Lakini watu wamekuwa wakinunua na kuuza bidhaa mbalimbali bila kuchukua tahadhari zozote. Alfred Bishundu ni mmoja wa watumiaji wa soko hilo anasema wamekuwa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida kwenye soko hilo wakiamini kuwa Mungu atawalinda dhidi ya janga hilo.

Anasema wamekuwa aakifanya biashara zao kwa muda mrefu lakini hata baada ya kuibuka kwa janga la virusi vya corona hajawahi kuhisi tofauti yoyote katika afya zao.

Naye Bi Mireyo Gwasa anayefanya biashara ya vinywaji baridi na moto katika soko la Mwibambo anasema baadhi ya watu wamekuwa wakijihadhari kwa kuepuka kusogeleana katika eneo hilo lakini wengi wao ni kama wanapuuzia kwa madai kuwa ugonjwa wa Covid-19 haujashamiri katika eneo hilo licha ya kuwa kitaifa tatizo hilo lipo.

Hali yaripotiwa kuwa tofauti kidogo katika soko la mkoa wa Ngozi Burundi

Baadhi ya wakaaazi wa Dar es Salaam baadhi wakivalia barakoa kujikingana virusi vya corona Picha: DW/E. Boniphace

Wakati hali ikiwa hivyo kwenye soko la Mwibambo wilaya ya Giteranyi mkoa wa Muyinga, hali ni tofauti kidogo katika soko la mkoa wa Ngozi nchini Burundi baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo na wateja wao wanachukua tahadhari kiasi.

Bw Hakizimana Abdullah ni muuzaji wa dawa za binadamu katika duka la dawa lililo kwenye soko la Ngozi anasema katika duka lake anazingatia kanuni za afya dhidi ya maambukizi ya Corona kwa kuwa ni amri ya serikali inayopaswa kufuatwa.

Hata hivyo anasema baadhi ya wateja wake wamekuwa wakifika kupata huduma bila kujavaa barakoa lakini amekuwa akiwalazimisha kunawa mikono kwa maji na sabuni vilivyo kwenye ndoo nje ya duka lake kabla ya kuwapa huduma yoyote.

Naye Bw Ngamira Kulira anayejishughulisha na utengenezaji wa simu mbovu kwenye soko la Ngozi anasema kwa siku anahudumia wateja zaidi ya 40 lakini baadhi yao hawavai barakoa na kwamba hali hiyo imekuwa ikimkosesha riziki kwani baadhi ya wateja huondoka baada ya kutakiwa kunawa ama kuvaa barakoa.

Mkuu wa wilaya ya Ruhororo Bi Birukundi Mamerte anasema serikali yake imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watu wanazingatia kanuni zilizotolewa na wizara ya afya kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya corona kwenye maeneo yote yenye mikusanyiko.

Bi Mamerte anasema tangu kuzuka kwa mlipuko wa Corona mwishoni mwa mwaka 2019, wilaya yake imepata kesi mbili pekee ambapo wagonjwa hao wote wamepona na kuruhusiwa na tangu February 10 mwaka huu wilaya hiyo haijapata kesi nyingine yoyote ya Corona.

Kuanzia January 11 mwaka huu, Serikali ya Burundi ilitangaza kufunga mipaka yake ya majini na ardhini kufuatia ongezeko kubwa la watu wanaopatikana na virusi vya corona.

Mwandishi: Seif Upupu, DW

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW