Hali ya dharura yatangazwa Liberia
7 Agosti 2014Rais Johnson Sirleaf amesema hali hiyo ya dharura itadumu kwa siku 90. Hii leo bunge la nchi hiyo linakutana kuridhia hatua hiyo ya hali ya dharura. Takriban raia 300 wa Laiberia tayari wameshaambukizwa virusi hivyo vya ebola na nusu ya wale walioambukizwa wameshafariki.
Rais huyo wa Liberia pia amewatolea mwito raia wake kufunga na kuliombea taifa kwa siku tatu kutokana na mripuko wa Ebola. Naye Makamu wa rais wa Liberia Joseph Bokai amesema hali ya dharura itasaidia kutoa nafasi ya nchi hiyo kukabiliana vilivyo na Ebola.
"Madaktari wa afya walikuwa hawapati nafasi ya kuwashughulikia wagonjwa kutokana na wao kuambukiwa, kwa hivyo tulitaka kudhibiti mienendo ya watu ili kupata nafasi ya kudhibiti ugonjwa huu, nadhani hali ya dharura ni sawa itatupa nafasi kukabiliana vilivyo", alisema Makamu wa rais Joseph Bokai.
Aidha shirika la afya ulimwenguni WHO linaloendelea na vikao vyake mjini Geneva juu ya suala hilo, jana Jumatano lilisema idadi jumla ya waliofariki imefikia watu 932 tangu kuanza mwaka huu huku watu 1,711 wakithibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo wa Ebola, katika mataifa ya Afrika Magharibi yanayopambana na janga hilo mbayo ni Guinea, Siera leone na Liberia.
Hata hivyo kumekuwa na wasiwasi wa kusambaa kwa ugonjwa huo nchini Naigeria baada ya vifo vya watu wawili miongoni mwa watu 7 waliogundulika kuambukizwa mjini Lagos nchini humo.
Huenda dawa ya Ebola ikapatikana
Huku kukiwa na waathirika wengi wanaougua ugonjwa wa Ebola barani Afrika wataalamu wa kiafya nchini Marekani wako mbioni kutafuta chanjo ya kuutibu huku watafiti wakisisitiziwa kuharakisha utafiti wao.
Watafiti wanasema dawa za majaribio walizopewa wamarekani wawili waliorejeshwa nyumbani kwa matibabu baada ya kuambukizwa ugonjwa wa Ebola nchini Liberia, wameonyesha dalili za kupata nafuu.
Lakini Rais Barrack Obama akizungumza katika mkutano wake na viongozi wa bara la Afrika uliomalizika hapo jana, alisema kwa sasa ni mapema mno kutoa dawa za majaribio kwa wagonjwa wa Ebola. Amesema pia hakuna maelezo ya kutosha juu ya dawa hizo hali inayomzuwiya kuridhia zianze kutumika kama dawa rasmi za kuutibu ugonjwa wa Ebola unaosemekana kutokea katika maeneo ya vijijini nchini Guinea.
Huku hayo yakiarifiwa wizara ya ulinzi ya Uhispania imesema padri wa kimishonari aliyeambukizwa ebola nchini Laiberia amewasili nchini humo kwa matibabu zaidi. Padri huyo Miguel Pajares, atapokea matibabu yake katika hospitali moja mjini Madrid. Pajares, aliambukizwa Ebola alipokuwa anasaidia kutoa matibabu kwa watu walioambukizwa Liberia.
Ebola inayosemekana kutoka kwa popo iligundulika kwa mara ya kwanza katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo mwaka wa 1976. unaweza kuupata ugonjwa huo kwa kushika majimaji ya mgonjwa aliyeambukizwa.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu