Hali ya haki za binaadamu bado kuboreka nchini Cuba.
8 Julai 2007Repoti ya shirika la haki za binaadamu la upinzani nchini humo haioni mabadiliko yoyote yale ya kuboreka kwa hali ya haki za binaadamu nchini Cuba.
Waraka uliotolewa kwa waandishi wa habari wa kigeni na Tume ya Haki za Binaadamu na Usuluhishi wa Kitaifa nchini Cuba inaelezea hali ya haki za binaadamu nchini Cuba kuwa mbaya kabisa katika Amerika ya Kaskazini.
Kwa mujibu wa tume hiyo haki zilizokuwa zikikiukwa ni pamoja uhuru wa kutowa maoni,uhuru wa kujiunga na vyama na uhuru wa vyombo vya habari na wa kujieleza pamoja na haki ya kuunda vyama vya wafanyakazi na makundi ya kisiasa au kufanya kazi nje ya mfumo wa ulezi wa kinyonyaji wa taifa hilo la kidikteta.
Ukiwa umesainiwa na waangalizi wa haki za binaadamu Elizardo Sanchez na Carlos J.Menendez waraka huo umesambazwa pamoja na repoti ya shirika la upinzani ya miezi sita juu ya wafungwa wa kisiasa na wafungwa wa itikadi orodha mbayo imeiandaa kutokana na habari kutoka kwa familia za wafungwa.
Juu ya kwamba orodha ya wafungwa wa kisiasa imeshuka kutoka wafungwa 283 kufikia mwishoni mwa mwaka 2006 hadi wafungwa 246 kufikia tarehe 30 mwezi wa Juni mwaka 2007 tume ya haki za binaadamu nchini Cuba inasema ni jambo lisilokuwa na ufafanuzi inakuwaje kuna wafungwa zaidi ya 200 katika nchi kama Cuba ambayo imeorodheshwa kuwa mojawapo ya nchi zisizokuwa na ghasia za kisiasa duniani.
Tokea kuanza kwa serikali ya mpito ya Raul Castro ambaye ni waziri wa ulinzi na ni kaka wa rais hakuna hata hatua moja iliochukuliwa katika kuufanya mfumo wa sheria kuwa wa kisasa.
Serikali ya Cuba haitambuwi uhalali wa repoti za aina hiyo ambapo kwa mujibu wa serikali ni za mashirika yasio na ushawishi nchini humo na yameweza kuendelea kuwepo kwa sababu yanaendelezwa na kufadhiliwa na serikali ya Marekani.
Mojawapo ya masuala ya haki za binaadamu yanayotajwa na wizara ya mambo ya nje ni mafanikio ya kijamii nchini Cuba na hakikisho wanalopatiwa watu wake milioni 11.2 katika fani ya elimu,afya na ajira.
Kutokuwepo kwa haki nyenginezo kunatajwa rasmi kuwa kunatokana na haja ya nchi hiyo kujihami dhidi ya serikali ya kigeni ambayo ni Marekani yenye kuchochea machafuko ya ndani ya nchi na kutangaza hadharani kwamba inaunga mkono mabadiliko ya serikali na mfumo katika kisiwa hicho.
Cuesta Morua msemaji wa Arco Progresista muungano wa makundi ya ujamaa na demokrasia anaona kumekuwepo na upunguzaji wa makali katika nyanja ya haki za binaadamu hususan katika kushughulikia sekta za upinzani kulinganisha na kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2006.
Anasema ni muhimu wa kupigiwa mfano kutambuliwa kwa tafauti zote ikiwa ni pamoja na tafauti za itikadi na maoni nchini hmuo.
Katika miezi ya hivi karibuni Cuba pia imeregeza masharti ya kusafiri nje juu ya kwamba hatua hiyo inahusu sekta fulani tu za wananchi wa Cuba.
Hata hivyo waraka wa Tume ya Haki za Binaadamu na Usuluhishi wa Kitaifa nchini humo unasema Cuba bado ni taifa la kidikteta na umbile lake linajitokeza katika kila fani ya maisha yake ya taifa kwa mfano katika suala la kujiajiri,kuwepo kikomo katika mawasiliano ya mtandao na adhabu kwa wale wanaojaribu kinyume na sheria kuangalia vituo vya televisheni vya kigeni.