1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya hatari yatangazwa Misri

MjahidA14 Agosti 2013

Huku Misri ikitangaza hali ya hatari, Uturuki imelihimiza Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Jumuiya ya nchi za kiarabu kupata suluhu ya haraka ya kusimamisha mauaji ya halaiki yanayofanyika nchini Misri.

Jeshi nchini Misri
Jeshi nchini MisriPicha: Reuters

Kulingana na Rais wa Mpito nchini humo Adly Mansour aliyetangaza hali ya hatari kote nchini Misri ametoa amri kwa jeshi la nchi hiyo kutoa usaidizi kwa polisi katika juhudi za kuhakikisha kuwa kunakuwa na hali ya utangamano nchini humo. Hali hiyo ya hatari inatarajiwa kuwepo kwa muda wa mwezi mmoja.

Vikosi vya serikali ya mpito nchini Misri vilivamia kambi za wakimbizi katika eneo la Rabaa Al Adawiya Kakaszini Mashariki mwa mji wa Cairo ambako waandamanaji walikuwa wamepiga kambi wakiapa kukaa katika eneo hilo hadi Mohammed Musri atakaporejeshwa tena madarakani kama rais halali wa Misri.

Ghasia MisriPicha: picture-alliance/dpa

Hali hii imezua ghasia katika miji mingine ya Minya Assiut na Alexandria.

Katika ghasia hizo za leo watu zaidi ya 90 wameuwawawa huku wengine wengi wakipata majeraha mabaya.

Kati ya waliouwawa ni mtoto wa kike wa Mohamed El-Beltagi, kiongozi wa chama cha Udugu wa Kiislamu chake Mohammed Musri na mpiga picha wa shirika la habari la Sky News, Mick Deane, aliye na umri wa miaka 61 aliyeuwawa kwa kupigwa risasi wakati alipokuwa kazini.

Viongozi wa Ulaya watoa tamko juu ya Misri

Kutokana na ghasia za leo, viongozi wa Ulaya wamelaani kitendo kilichofanywa na vikosi hivyo dhidi ya kambi za waandamanaji mjini Cairo.

Viongozi hao sasa wametaka kuwepo kwa mazungumzo ya amani haraka iwezekanavyo ili kuirudisha Misri katika hali ya utulivu.

Waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema ni wazi kuwa kutokana na jamii ya Kimataifa kuunga mkono tangu mwanzo, hali iliyokuwa ikiendelea nchini humo baada ya kuondolewa uongozini kwa Mohammed Mursi ndio sababu kuu ya kutokea kwa shambulizi la leo dhidi ya waandamanaji.

Waziri wa nchi za nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: picture-alliance/dpa

Erdogan amesema jamii hiyo ya Kimataifa sasa hasa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Jumuiya ya nchi za kiarabu zinapaswa kuja na suluhu ya haraka ili kumaliza mauaji yanayofanyika huko.

Miito zaidi ya amani Misri

Hata hivyo Peter Stano msemaji wa Umoja wa Ulaya amesema hawaungi mkono kile kinachoendelea Misri kwa sasa na kwamba wana wasiwasi mkubwa juu ya idadi ya vifo inayoendelea kupanda kutokana na machafuko ya leo.

Naye waziri wa mambo ya nje nchini Ujerumani, Guido Westewelle, amehimiza vyama vyote kuja pamoja ili kufikia maelewano juu ya mustakbali wa Misri.

Marekani pia imetoa sauti yake juu ya ghasia za Misri kwa kusema kuwa haiungi mkono hali ya hatari iliotangazwa na viongozi wa jeshi la Misri.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: Reuters

Msemaji wa ikulu ya Marekani Josh Earnest, aliyekuwa akiwahutubia vyombo vya habari wakati Rais wa Marekanni Barrack Obama akiwa mapumzikoni kwa siku nane alisema kuwa Misri lazima iheshimu haki za inaadamu ya raia wake.

Wakati huo huo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelaani vikali mauaji nchini Misri na kutaka mazungumzo ya amani yafanyike mara moja.

Mwandishi: Amina Abubakar/(dpa)/Reuters/APE/AFP

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW