Hali ya hatari yatangazwa Pakistan
4 Novemba 2007Katiba ya nchi imeahirishwa na askari polisi wamezingira jengo la Mahakamu Kuu mjini Islamabad na Jaji Mkuu Ifitkar Chaudhry ameondoshwa kazini.Mahakama Kuu ilitazamiwa kutoa hukumu yake siku ya Jumanne juu ya uhalali wa kumteua Musharraf mwezi uliopita, kugombea tena uchaguzi wa rais huku akishika madaraka ya kijeshi.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Pakistan PPP, Bibi Benazir Bhutto amesema,anakubaliana na Jemadari Musharraf kuwa kuna kitisho cha wafuasi wa itikadi kali kujiimarisha,lakini wasiwasi wake ni kuwa hali hiyo imezuka wakati wa utawala wa Musharraf.Anasema,ikiwa serikali haitobadilishwa basi wafuasi wa itikadi kali watajiimarisha.
Ripoti zinasema,wanasheria na wanasiasa wa upinzani wapatao kama dazeni moja wamekamatwa. Hivi sasa haijulikani kama uchaguzi wa bunge utafanywa mwezi wa Januari kama ilivyopangwa hapo awali.