1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya kibinaadamu yazidi kuwa mbaya Gaza

10 Mei 2024

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 100,000 wamelazimika kuondoka katika mji wa Rafah unaokabiliwa na kitisho cha kushambuliwa na Israel na hatari ya kukumbwa na njaa kutokana na uhaba wa misaada ya chakula.

Mzozo wa Gaza | Rafah
Moshi ukifuka huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza: 07.05.2024Picha: Ramez Habboub/AP Photo/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema hata asiposaidiwa na nchi yoyote, wataendeleza operesheni yao ya kijeshi huko Gaza hadi kulitokomeza kabisa kundi la Hamas ambalo limeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya Magharibi kama kundi la kigaidi.

Siku ya Alhamisi,  Netanyahu  alisema kuwa kitisho cha Marekani cha kuzuia kuipatia Israel baadhi ya silaha hakitazuia kutanuwa mashambulizi yake huko Gaza ambayo kwa sasa yamejikita zaidi kwenye mji wa Rafah. Mapema wiki hii Israel ilichukua udhibiti wa kivuko cha Rafah kinachopakana na Misri, na hivyo kusababisha mgogoro mkubwa katika shughuli za kibinadamu.

Mfanyakazi wa Shirika la Kimataifa la kuwasaidi wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) akisimamia usafirishaji wa misaada huko Gaza.Picha: Mohammed Abed/AFP/Getty Images

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, limefahamisha kuwa hadi kufikia kesho Jumamosi, litashindwa kabisa kuendelea na zoezi la usambazaji chakula ikiwa misaada zaidi haitowasilishwa eneo hilo la kusini mwa Gaza la Rafah linalowahifadhi Wapalestina karibu milioni 1.3 ikiwa ni zaidi ya nusu ya wakazi wote wa Gaza.

Soma pia: WHO: Gaza bado inakabiliwa na kitisho cha njaa

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameonya hivi leo kuwa eneo la kaskazini mwa Gaza tayari linashuhudia hali kamili ya "baa la njaa"  na kwamba shughuli za kuingiza misaada huko Gaza zinaweza kusitishwa kwa siku kadhaa kufuatia uamuzi wa Israel kuushambulia mji wa Rafah licha ya miito ya Jumuiya Jumuiya ya kimataifa kuitaka kuachana na azma hiyo.

Maafisa hao wameongeza kuwa ukosefu wa bidhaa ya mafuta unadhoofisha miundombuni ya afya pamoja na mifumo ya maji safi na maji taka kote katika ukanda wa Gaza.

Wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya leo Ijumaa kuwa operesheni kamili ya ardhini ya Israel huko Rafah itasababisha "janga kubwa la kibinadamu". Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa ziara yake katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Guterres amesema:

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Picha: ZUMA Wire/IMAGO

" Takriban Wapalestina laki moja wanahamia eneo la Kaskazini wakitokea Rafah, lakini mashirika ya kibinadamu hayana mahema au akiba ya chakula vilivyosalia kusini mwa Gaza. Shambulio kubwa la ardhini huko Rafah, litasababisha maafa makubwa ya kibinadamu na kukwamisha juhudi zetu za kuwasaidia watu huku njaa ikiwanyemelea. Sheria ya kimataifa ya kibinadamu iko wazi kabisa, raia ni lazima walindwe."

Soma pia: Mapigano makali na milipuko yautikisa Ukanda wa Gaza

Hayo yanaripotiwa wakati wapatanishi wameshindwa kufikia muafaka katika mazungumzo ya kusaka mkataba wa usitishwaji mapigano yaliyokuwa yakiendelea mjini Cairo nchini Misri. Vita hivi vilivyoanza Oktoba 7 baada ya shambulizi baya la Hamas kusini mwa Israel, tayari vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 34,500 huku maelfu ya wengine wakijeruhiwa, hii ikiwa ni kulingana na Wizara ya afya inayodhibitiwa na  kundi la Hamas.

Pia, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linatazamiwa hii leo kuipigia kura rasimu ya azimio ambalo huenda itaipatia Palestina uwakilishi mkubwa na haki zaidi ya ushiriki katika vikao vya Baraza hilo.

(Vyanzo: Mashirika)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW