1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya kibinadamu yaendelea kuwa ngumu Sudan

Josephat Charo
22 Oktoba 2025

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu OCHA imeripoti kwamba ongezeko la machafuko linakoleza hali ngumu ya kibinadamu inayoshuhudiwa katika jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan.

Machafuko yanayoendelea Sudan yanakoleza hali ngumu ya kibinadamu
Machafuko yanayoendelea Sudan yanakoleza hali ngumu ya kibinadamuPicha: UNICEF/Xinhua/picture alliance

Farhan Haq, naibu msemaji wa wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema katika mji wa Tawila, timu ya OCHA ilikutana na familia ambazo zilitembea kwa siku nne kukimbia ghasia katika mji mkuu wa jimbo uliozingirwa wa El Fasher, ambao uko umbali wa kilomita 50. Siku ya Jumapili na Jumatatu pekee, baadhi ya familia 350 - wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee - walifika wakiwa katika hali mbaya, baadhi yao walijeruhiwa njiani.

Washirika wa OCHA wanaotoa misaada ya kibinadamu wametoa chakula, maji na huduma ya msingi ya matibabu kwa waliowasili, lakini kunahitajika rasilimali zaidi kuliko zile zilizopo kwa sasa. Mji wa Tawila sasa unakaribisha zaidi ya watu 600,000 waliokimbia makazi yao kutoka El Fasher na maeneo jirani - na familia nyingi zilizokimbia hazina makazi, chakula cha kutosha au maji salama. OCHA inaratibu utoaji wa misaada ikishirikiana na mamlaka, wafadhili na washirika wa ziada.

Haq ameongeza kusema katika eneo la El Fasher, mashambulizi ya mara kwa mara yanaendelea kuhatarisha maisha ya raia. Vyanzo vya ndani vinaripoti kwamba jana Jumanne, makombora makubwa yalipiga maeneo ya kati ya jiji hilo, na kuhatarisha maelfu ya raia katika moja ya maeneo yenye watu wengi zaidi ya El Fasher.

Mamlaka za mitaa zinaripoti kwamba zaidi ya watu 109,000 wameyahama makazi yao katika maeneo 127, wengi wao wakikosa huduma za matibabu kwa sababu ya kufungwa kwa maji na majiko kadhaa ya kijamii wiki iliyopita kutokana na kukosekana mahitaji ya vyakula. Kwa mara nyingine tena, OCHA inasisitiza kwamba mzingiro wa El Fasher lazima uondolewe mara moja, na upitishaji salama lazima uhakikishwe kwa raia wanaotaka kukimbia na kwa maafisa wasaidizi wa mashirika ya misaada walioazimia kutoa misaada muhimu.

Watoto ni miongoni mwa waathiriwa wa machafuko yanayoendelea nchini SudanPicha: DW

Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu, Umoja wa Mataifa alisema, "Tukiigeukia Sudan, Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu inaripoti kwamba wakati machafuko yanaongeza janga baya la kibinadamu katika jimbo la Darfur Kaskazini. Sisi na washirika wetu tunaendelea kuongeza juhudi zetu za kukabiliana na hali hii na kupeleka misaada katika maeneo ambako ufikiaji unaruhusu."

Kwingine huko Darfur Kaskazini, shambulizi la ndege zisizo na rubani limeripotiwa kulilenga soko kuu katika mji wa Kabkabiya, na kudhihirisha hatari kubwa zinazowakabili raia wakati mapigano yanazidi kuongezeka.

Uwanja wa ndege wa Khartoum washambuliwa

Wakati huo huo, chanzo cha kijeshi cha Sudan kmeliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba ndege zisizo na rubani za kijeshi zililenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum siku ya Jumatano kwa siku ya pili mfululizo.

Chanzo hicho, ambacho kilizungumza bila kutajwa jina kwa sababu hakikuwa na idhini ya kutoa taarifa kwa vyombo vya habari, kilisema "ndege zisizo na rubani ziliulenga uwanja wa ndege wa Khartoum kwa mara nyingine alfajiri" siku ya Jumatano. Aliongeza kuwa ulinzi wa anga wa jeshi ulizuia ndege zisizo na rubani alizosema kuwa zilirushwa na "kundi la magaidi waasi" -- akizungumzia kikosi cha wapiganajji wanamgambo wa Rapid Support Forces RSF ambalo limekuwa likipigana na jeshi la Sudan tangu Aprili 2023.

Uwanja wa ndege wa Khartoum umeshambuliwa na kukwamisha ufunguzi wakePicha: El Tayeb Siddig/REUTERS

Mamlaka ya usafiri wa anga ya Sudan ilikuwa imesema uwanja huo wa ndege utafunguliwa tena Jumatano, huku safari za ndege za ndani zikirejea hatua kwa hatua baada ya maandalizi ya kiufundi na kiutendaji kukamilika. Lakini kufunguliwa tena kwa uwanja huo kumeahirishwa baada ya shambulio la Jumanne. Safari ya kwanza ya kibiashara ya ndege ndani ya nchi ya shirika la ndege la Badr ilikuwa imepangwa Jumanne Oktoba 22.

Siku ya Jumanne, mashahidi waliripoti kusikia milipuko mingi katika eneo karibu na uwanja wa ndege mapema asubuhi. Kituo hicho kilionekana kuwa sawa wakati wa ziara ya baadaye siku hiyo ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan. Akizungumza kutoka ndani ya uwanja wa ndege, Burhan alisema jeshi "limedhamiria kuuangamiza uasi huu wa kundi la RSFliinaloongozwa na mshirika wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.

RSF haijadai kuhusika na mashambulizi hayo, lakini imekuwa ikishutumiwa mara kwa mara kwa kutumia ndege zisizo na rubani kulenga miundombinu ya kijeshi na kiraia katika miezi ya hivi karibuni. Katika hotuba iliyotolewa Jumanne jioni kwenye mtandao wa kijamii, Daglo alidai RSF "hushambulia maeneo ya kijeshi pekee" na kuapa kuliangamiza jeshi, ambalo aliliita "saratani".

OCHA inasisitiza wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wa kukomesha uhasama mara moja kote Sudan, kuimarisha ulinzi wa raia na miundombinu ya kiraia, na ufikiaji usiozuiliwa wa kibinadamu kwa wale wote wanaohitaji.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW