Hali ya kisiasa i tete Lebanon
26 Januari 2011Usalama umeimarishwa na shule kadhaa bado zimefungwa baada ya maandamano ya jana.Polisi wa kupambana na ghasia wanapiga doria katika eneo la Tripoli anakotokea Waziri Mkuu mteule Najib Mikati ambaye ni msuni.Ijapokuwa Najib Mikati ni Msunni,uteuzi huo umezua hisia tofauti kati ya WaSunni wanaoamini kuwa ni harakati za Hezbollah za kutaka kuwa na ushawishi mkubwa serikalini.
Pindi baada ya kuteuliwa na Rais Michel Sleiman hapo jana,Najib Mikati alisisitiza kuwa azma yake ni kuwashirikisha wadau wote kwa madhumuni ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na wala sio kuyapa kipa umbele maslahi ya Hezbollah na kuwasihi ,"Tafadhali musiwe na dhana zozote mbaya dhidi yangu wala utendaji wangu…hasa katika jamii ya kimataifa.Nayasema haya kwa kweli yote...mapendekezo ya Hezbollah kamwe hayana ishara kuwa lazima niyatimize matakwa yao ya kisiasa…..ila wajibu wangu ni kuyatimiza malengo ya kitaifa."alifafanua.
WaSunni wajawa na ghadhabu
Uteuzi huo uliofanywa baada ya Saad Hariri kujiuzulu hivi karibuni ulisababisha ghadhabu na kuwachagiza Wasunni kuandamana katika eneo la Tripoli lililo na Wasunni wengi. Kulingana na makubaliano ya kugawana madaraka yaliyofikiwa kati ya kambi tofauti za kisiasa,Waziri Mkuu wa Lebanon sharti awe Msunni.Hatua hiyo imewatia wasiwasi pia viongozi wa Ufaransa na Marekani waliotoa wito wa kujizuwia na kudumisha amani.Kauli hizo zinaungwa mkono na Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa UIaya Catherine Ashton aliyeusisitizia umuhimu wa wahusika wote kushirikiana.
Hezbollah na mabavu
Kwa upande wake Marekani inalilaumu kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran na Syria,kuwa linatumia mabavu kuwa na ushawishi mkubwa serikalini.Itakumbukwa kuwa mvutano uliojitokeza katika serikali ya Lebanon ulichochewa na shinikizo za kumtaka Waziri Mkuu wa zamani Saad Hariri kutoitambua Mahakama maalum inayoyachunguza mauaji ya marehemu babake Rafiq Hariri yaliyotokea mwaka 2005.Kwa mtazamo wa Hezbollah,baadhi ya wanachama wake huenda wakatiwa hatiani kwa tuhuma za kuhusika katika njama hiyo.
Suala tete la mahakama
Kuhusu suala hilo,Najib Mikati alisema kuwa atafanya kila awezalo ili kulishughulikia suala hilo kwa majadiliano.Bila ya ufafanuzi zaidi, alisisitiza kuwa Lebanon haina uamuzi wowote katika operesheni za mahakama hiyo ya kimataifa ila ushirikiano wake ni suala jengine.Ifahamike kuwa mpaka sasa orodha kamili ya majina ya watuhumiwa wa mauaji hayo ya marehemu Rafiq Hariri bado hayajatangazwa.Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya Kiarabu Amyr Moussa amesema kuwa ,"Tunaupa umuhimu mkubwa ustawi wa Lebanon na tutaendelea kufanya kila tuwezalo mpaka hali ya kawaida itakaporejea."
Marekani imetahadharisha kuwa endapo Lebanon itaongozwa na Hezbollah,uhusiano kati ya mataifa hayo mawili utaathirika.
Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/DPAE
Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhani