1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya kisiasa inazidi kutokota Iraq

Mjahida11 Agosti 2014

Marekani imesema inatafuta mbinu mpya ya kuwahamisha maelfu ya wairaqi kutoka jamii ya Yazidi waliokwama katika maeneo ya milima, Kaskazini mwa Iraq kufuatia mashambulizi ya waasi wa dola la Kiislamu (IS)

Baadhi ya jamii ya Yazidi ikikimbia mashambulizi ya waasi wa IS Iraq.
Baadhi ya jamii ya Yazidi ikikimbia mashambulizi ya waasi wa IS Iraq.Picha: Reuters

Huku hatua ya kuwadondoshea chakula raia wa Iraq waliokwama katika eneo la Sinjar ikionekana kuwapa msaada uliokuwa unahitajika kwa kiwango kikubwa, bado hali ya mazingira katika mlima Sinjar imesababisha mauaji ya wengi kutoka jamii ya wachache ya Yazidi wanaotishiwa na mashambulizi kutoka kwa waasi wa dola la kiislamu.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters Mshauri wa usalama wa kitaifa wa Marekani Ben Rhodes amesema wanaangalia hatua za kuchukua za kuwaondoa wakaazi waliobakia katika maeneo ya milima.

Rhodes amesema vikosi vya kikurdi vinasaidia katika hilo na wanaendelea na mazungumzo na Umoja wa Mataifa pamoja na washirika wengine wa Kimataifa kuona ni kwa njia gani wanaweza kuwaleta jamii ya Yazidi katika eneo salama.

Mshauri wa usalama wa kitaifa wa Marekani Ben Rhodes.Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Jamii hiyo ni wafuasi wa imani ya kale wanaoonekana na waasi wa kisuni kama watu walio na imani ya kishetani na kwa sasa wanalazimishwa kuingia katika dini ya kiislamu au wauwawe.

Habari nyengine ni kwamba katika siku mbili ya mapigano kati ya waasi wa IS na vikosi vya kurdi katika eneo la Jalawla yamesababisha mauaji ya watu kumi huku wengine zaidi ya 80 wakijeruhiwa. Kundi hilo kwa sasa limechukua udhibiti kamili wa eneo hilo la Jalawla.

Maliki kupambana mahakamani, kuulinda wadhifa wake

Huku hayo yakiarifiwa Waziri Mkuu wa Iraq Nouri Al Maliki anapeleka vita vyake vya kuuulinda wadhifa wake mahakamani, baada ya kutangaza kwamba atachukua hatua za kisheria dhidi ya rais mpya wa nchi hiyo, Fuad Massoum, kwa kukiuka katiba, kutokana na kushindwa kumpa waziri mkuu kutoka kundi kubwa zaidi la wabunge bungeni jukumu la kuunda serikali, mpya.

"Rais fuad Massoum hana haki kuchelewesha uteuzi wa waziri mkuu kutokana na matokeo ya uchaguzi uliopita, hali hii itazidisha matatizo ya kiusalama, ndio maana serikali inakwenda kotini kumshaki rais kwa kukiuka katiba," alisema Maliki.

Hata hivyo mahakama ya juu nchini humo imemuunga mkono Maliki katika harakati zake za kutaka kuiongoza tena nchi hiyo kwa muhula wa tatu.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al Maliki.Picha: Brendan Smialowski/AFP/Getty Images

Vyombo vya habari nchini humo Mahakama hiyo imeamua kwamba kulingana na sheria muungano wa Maliki walio wengi bungeni ndio walio na haki ya kupema jukumu la kuunda serikali, kwa hiyo rais Fouad Massoum atakuwa hana budi ila kumpa Maliki jukumu la kuunda serikali mpya.

Kwa upande wake Marekani inayounga mkono hatua ya rais mpya imesema inatumai Nouri al Maliki hataingilia siasa za nchi hiyo.

Marekani kupitia waziri wake wa mambo ya nje John Kerry imesema kuundwa kwa serikali ni hatua muhimu ya kuwepo kwa udhabiti na usalama nchini humo huku akiongeza kwamba kitu wananchi wanachokitaka kwa sasa ni amani kwa hiyo nguvu kupita kiasi hazipaswi kutumiwa na makundi ya kisiasa wakati huu wa kipindi cha demokrasia kwa Iraq.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/dpa/AP

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW