1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya kisiasa Zimbabwe

Mwagodi24 Juni 2008

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limelaani unyanyasaji dhidi ya upinzani nchini Zimbabwe huku katibu mkuu Ban Ki Moon akimtaka rais Mugabe kutoendelea na uchaguzi huo Ijumaa ijayo.

Morgan Tsvangirai,kiongozi wa chama cha MDCPicha: AP


Hayo yakijiri, bado Kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai amejificha katika ubalozi wa Uholanzi kwa kuhofia usalama wake, baada ya kujiondoa kwenye duru ya pili ya uchaguzi.

Akizungumza na waandishi habari baada ya mkutano wa mataifa 15 wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa,Ban Ki Moon, alisema hatua ya Morgan Tsvangirai kujiondoa katika uchaguzi inaeleweka kutokana na mgogoro unaogubika Zimbabwe. Ban alisema wangemrai rais Mugabe kutoendelea na duru ya pili ya uchaguzi,kwani utagawanya wananchi na kusababisha vurugu zaidi. Baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa,limeskitishwa na hujuma dhidi ya wafuasi wa upinzani. Bila kumlaumu Mugabe,Ban alisema, hali nchini Zimbabwe inatishia usalama wa mataifa ya kusini mwa Afrika.


Hatahivyo,mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Zimbabwe, George Chiweshe amesema uchaguzi huo lazima uendelee kwani hakuna vita nchini humo.


Na kwa mara ya kwanza,China imezungumzia juu ya mgogoro wa Zimbabwe.

Msemaji wa waziri wa mambo ya nje Liu Jianchao aliwaambia waandishi habari kwamba wanamatumaini upande wa serikali na upinzani watatumia njia za kidiplomasia kutatua mgogoro uliopo.

Tsvangirai ajificha


Hadi sasa bado Tsvangirai yuko katika ubalozi wa Uholanzi mjini Harare . Alikimbilia huko jana kwa usalama wake baada ya makao makuu ya afisi ya MDC ilipovamiwa na maafisa wa polisi, ambao waliwakamatwa wafuasi wao 60 waliokuwa wametafuta hifadhi katika afisi hiyo.Kati ya waliokamatwa walikuwemo akina mama na watoto.


Maafisa wa ubalozi huo wamesema Tsvangirai hajaomba hifadhi ya kisiasa lakini wataendelea kumhifadhi hadi atakapohakikishiwa usalama wake.Tsvangirai amesema ataondoka katika masaa 48 yajayo baada ya kupokea hakikisho la usalama wake na serikali ya Mugabe.


Kamishna mkuu a polisi wa Zimbabwe,jenerali Augustine Chihuri alisema wameshangazwa na hatua ya Morgan Tsvangirai na kuitaja kama mkakati wa kuchafua sura ya Zimbabwe kimataifa ili kuzuia uchaguzi, ''Tunashangaa Tsvangirai anamtoroka nani?'' Hatahivyo kumekuweko na uvumi juu ya njama za kutaka kumuuwa Tsvangirai

Juhudi za kidiplomasia

Kwengineko mawaziri wa mambo ya nje wanachama wa SADC,wanaendelea kulijadili swala la Zimbabwe katika mji mkuu wa Angola-Luanda. Waziri wa mambo ya nje wa Angola,Joao Bernardo de Miranda alisema, hali nchini Zimbabwe ni ya hatari na uchaguzi wa ijumaa hautakuwa wa haki.

Kadhalika, aliyekuwa mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini Bosnia Paddy Ashdon,amemtaka rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki kuzungumzia kwa kina tatizo la Zimbabwe na kumaliza kimya chake kuhusiana na visa vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyoendelea Zimbabwe. Ashdon aliyekana madai kwamba alipendekeza uvamizi wa kijeshi nchini humo,alisema pia bado kuna matumaini ya kuutatua mgogoro wa Zimbabwe kwa njia za kidiplomasia.




Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW