Hali ya Misri na matokeo ya uchaguzi wa Mali
16 Agosti 2013Hali nchini Misri na kitisho cha kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe,uchaguzi nchini Mali na mvutano kati ya waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Dirk Niebel na shirika la haki za binaadam la FIAN kuhusu kisa cha kupokonywa ardhi yao wakulima wadogo wadogo wa Uganda ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa Ujerumani kuhusu bara la Afrika katika kiüindi cha wiki moja iliyopita.
Tuanzie Misri ambako vuta vikuvute kati ya wafuasi wa rais aliyeng'olewa madarakani Mohammed Mursi na serikali ya mpito inayoungwa mkono na jeshi inaendelea na kuzusha hofu ya kuripuka vita vya wenyewe kwa wenyewe. Der Tagespiegel linajiuliza kama juhudi za kidiplomasia zimeshindwa na wapi inaelekea nchi hiyo ya mto Nile?
Der Tagesspiegel limezungumzia juhudi za waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle aliyekuwa waziri wa kwanza wa Umoja wa Ulaya kuitembelea Misri,baada ya ziara ya mwakilishi mkuu wa siasa ya nje wa Umoja wa ulaya,Catherine Ashton na naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani William Burns.Lengo la wanasiasa wote hao lilikuwa kuwatanabahisha viongozi wa Misri,kuanzia jenerali Abdel Fattah al Sissi,kupitia rais wa mpito Adly Mansur hadi kufikia waziri mkuu wa mpito Hazem al Belawi wasiendelee kutumia nguvu kumaliza mvutano pamoja na wafuasi wa udugu wa kiislam.Juhudi hizo hazijasaidia kitu,badala ya kuitishwa mazungumzo ya dhati pamoja na viongozi wa udugu wa kiislam wanaoshikiliwa korokoroni,jenerali Assisi amewatolea wito wananchi wamruhusu aendeleze mapambano dhidi ya magaidi.Matokeo yake :damu inaendelea kumwagika,mamia wanasemekana wameshapoteza maisha yao na maelefu kujeruhiwa huku Misri ikijikuta ukingoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.Der Tagespiegel linasema katika uhariri wake,wakristo wa madhehebu ya Koptik ndio wanaoathirika zaidi katika mzozo huu wa Misri.
Mali katika njia ya amani
Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamezungumzia pia kuhusu matumaini mema yaliyochomoza nchini Mali baada ya uchaguzi wa rais uliompatia ushindi Ibrahim Boubacak Keita-IBK.Mtu wa Ufaransa ashinda Mali" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Berliner Zeitung linalozungumzia jinsi wasimamizi wa nchi za magharibi walivyoridhika na jinsi uchaguzi huo ulivyopita.Gazeti hilo la mji mkuu limenukuu uhariri wa mkuu wa matangazo ya DW kwa bara la Afrika,Claus Stäcker" chini ya kichwa cha maneno"Mali imepiga kura inavyotakikana".Katika uhariri huo Claus Stäcker amesema rais wa Ufaransa Francois Hollande amempongeza Keita hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa na kumtaja IBK kuwa mtu wa kutegemewa na muaminifu.
Hata hivo gazeti hilo la mji mkuu limemnukuu pia mtaalam wa masuala ya Afrika,Dominic Johnson akitahadharisha na kusema "IBK-kifupisho cha jina la Ibrahim Boubacar Keita" atafanya makosa akiamini kwamba ushindi wake ni thibitisho la uungaji mkono wa msimamo wake wa kisiasa.Wamali wamepiga kura kutaka amani,kutaka wajipatie kiongozi mwenye nguvu ambae atakubaliwa tangu na wanajeshi mpaka na waasi wa tuareg-mtu wanaemuamini na mwenye uwezo wa kuiongoza nchi hiyo na ikihitajika kuhakikisha utulivu.Mali inahitaji mdahalo kati ya makundi tofauti ya kisiasa ili kuifumbua mizozo ya kila aina iliyoko na kusuluhisha pande zilizopigana vita katika eneo la kaskazini na pia kati ya makundi yanayohasimiana ya kisiasa katika mji mkuu Bamako.
FIAN yapigania haki ya wakulima wadogo wadogo wa Uganda
Mada yetu ya mwisho inahusu barua inayokosolewa vikali waliyoandikiwa wanaharakati wa shirika linalopigania haki za binaadam la FIAN na waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Dirk Niebel kuhusiana na kisa cha kutimuliwa katika ardhi yao wakulima wa Uganda.Dirk Niebel awakera wanaharakati wa shirika la misaada ya kiutu ndio kichwa cha maneno cha gazeti la die Tageszeitung kuhusu kisa cha kutimuliwa familia 400 za wakulima wadogo wadogo wa Uganda kutoka ardhi ya hekari 2512 katika mkoa wa Mubende na kuachiwa uwanja kampuni la kilimo cha kahawa Kaweeri Kafeeplantage ambalo ni tawi la kampuni la kahawa la Neumann Kaffee Gruppe lenye makao yake makuu mjini Hamburg.
Baada ya kuzungumzia barua waliyotumiwa FIAN na waziri wa misaada ya maendeleo,Dirk Niebel inayokosa harakati za FIAN kuwa zimekithiri na si za haki,pamoja na jibu la mwenyekiti wa FIAN,Ute Hausmann,die tageszeitung limetaja utayarifu wa mwenyekiti wa FIAN kuzungumza na waziri wa amisaada ya maendeleo na kumuomba azingatie hali inayowasibu wakulima hao waliotimuliwa.
Mwandishi Hamidou Oummilkheir/All Presse
Mhariri: Josephat Charo