Hali ya mpango wa chanjo za watoto duniani
3 Oktoba 2005Ripoti hiyo ya UNICEF ni ya tatu katika mpango wa shirika hilo la kufuatilia hali za watoto duniani, unaojulikana kama ‘Progress for Children’. Mpango huo unaorodhesha nchi kulingana na idadi ya watoto waliochanjwa nchini humo, kuanzia mwaka 1990.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo nchi 103 tayari zimeshachanja asilimia 90 ya watoto nchini mwao na mataifa mengine 16 yanaendelea vizuri na mipango yao ya chanjo.
Lakini nchi nyingine 74 haziaendelei vizuri na mipango ya chanjo na kuna nchi ambazo zinachelewesha utekelezaji wa mipango hiyo.
Bi. Ann Veneman, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, amesema karibu nchi zote zinazoendelea zimeweza kutokomeza kabisa magonjwa yanayoweza kuzuiliwa kwa chanjo.
Ameongeza kwamba kwa upande mwingine, eneo la Magharibi na Kati mwa Afrika, lenye asilimia 52 tu ya watoto waliochanjwa, ndio linaloongaza kwa idadi kubwa ya vifo vya watoto kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuiliwa kwa chanjo.
Baadhi ya magonjwa ya watoto yanayoweza kuzuiliwa kwa chanjo ni surua na mafua.
Tangu mwaka 1990 asilimia 70 ya watoto duniani wamechanjwa dhidi ya magonjwa mbalimbali. Mwaka 2002 wajumbe wa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa
walikubaliana mpango wa chanjo kwa takriban asilimia 90 ya watoto duniani, chini ya umri wa mwaka mmoja, ifikapo mwaka 2010.
Bi. Veneman amesisitiza kuna faida katika huduma za afya za kinga, mfano kuchanja watoto dhidi ya magonjwa mbalimbali. Amesema wanakadiria kuwa mwaka 2003 vifo vya watoto milioni mbili vilizuiliwa kutokana na chanjo.
Ameongeza kwamba mipango ya chanjo ina uwezo wa kuzuia vifo vya watoto, chini ya miaka mitano, kwa robo duniani kote kama asilimia 90 ya watoto watachanjwa.
Ripoti hiyo imesema ni lazima watoto wapewe chanjo kwa sababu, sio kama mipango mingine ya huduma za afya ambayo inasaidia tu watoto wasiumwe. Kwani chanjo inahakikisha watoto hawapati kabisa ugonjwa huo.
Dr. Peter Salama, kiongozi wa mpango wa chanjo UNICEF, amesisitiza hilo kwa kukumbushia kampeni dhidi ya ugonjwa wa kupooza. Alisema mwaka 1998 kulikuwa na wagonjwa 50,000 lakini leo hii kuna wagonjwa 1,300 tu.
Alisema kwamba ripoti hiyo inaonyesha ni muhimu nchi zote zijue kwamba wote tuko hatarini kama mipango ya chanjo haitakamilishwa.
Dr. Salama alisema jambo hili linamadhara makuu mawili, kwanza kuna hatari kwa magonjwa ambayo karibu yatokomezwe kabisa katika nchi zilizoendelea kuibika upya. Pili, wataalam sasa hivi bado wanendelea kusumbuka na magonjwa ya zamani na hivyo magonjwa mapya yanapoibuka hawakotayari kuyakabili kikamilifu.
Ripoti hiyo imesema maeneo yenye mipango mizuri ya chanjo ni pamoja na Amerika ya Kusini, visiwa vya Karibik, baadhi ya maeneo ya bara la Asia na mataifa mengi yalioendelea.
Maeneo yenye matatizo ni Magharibi na Kati mwa Afrika na Kusini mwa bara la Asia, maeneo yenye watoto wengi zaidi duniani.
Mfano nchi ya Nigeria, ingawa ina utajiri mkubwa wa mafuta, lakini mipango ya chanjo ya Nigeria inawafikia asilimia 35 tu ya watoto wa nchi hiyo.
Ripoti hiyo lakini inasema kwamba hali mbaya kama hizo zinaweza kubadilishwa. Mfano nchini Eritrea ambapo miaka kumi tu iliyopita watoto waliokuwa wanachanjwa walikuwa asilimia 18, lakini leo hii zaidi ya asilimia 80 ya watoto wanachanjwa. Na wakati huo huo Niger imeongeza idadi ya watoto wanaochanjwa kutoka asilimia 25 hadi 64. Nako nchini Uganda idadi imepanda kutoka asilimia 52 hadi 82.
Kampeni za chanjo zinaweza zisifanikiwe kwa sababu mbalimbali, ripoti hiyo imeeleza, kwa mfano nchi ikiwa na miundo mbinu duni, jamii zikiwa na imani potofu juu ya lengo la chanjo, imani za kitamaduni na kutokuwepo kwa wafanyakazi wa kutosha katika sekta ya afya.