1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Darfur Kaskazini yatishiwa na njaa kali

2 Agosti 2024

Hali ya njaa imesambaa kote katika jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan na huenda ikabaki hivyo hadi mwezi wote wa Oktoba kutokana na mzozo unaoendelea kwa zaidi ya miezi 15 na kulivuruga taifa hilo.

Sudan | Kitisho cha njaa
Hali ya njaa imesambaa kote katika jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan na huenda ikabaki hivyo hadi mwezi wote wa Oktoba kutokana na mzozo unaoendelea kwa zaidi ya miezi 15Picha: Luke Dray/Getty Images

Ripoti ya Shirika la usalama wa chakula la Food Security Phase Classification, IPC limegundua kwamba baadhi ya maeneo ya Darfur Kaskazini na hasa katika kambi ya Zamzam yanakabiliwa na aina mbaya kabisa ya njaa wanayooita IPC Awamu ya 5.

IPC inajumuisha mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa, makundi ya misaada na serikali ambazo hutumia ripoti zake kutathmini mizozo ya chakula na lishe ulimwenguni.

Na Awamu ya 5 ya IPC hufikiwa katika maeneo ambako angalu mtu mmoja kati ya watano ama hata makazi hukosa kabisa chakula na kuathirika na nhaa ama umaskini ambao huchochea utapiamlo mkali na hata kifo.

Mwezi Mei, Mpango wa Chakula Duniani, WFP uliripoti kwamba karibu watu milioni 1.7 walikuwa tayari wanakabiliwa na viwango vya kutisha vya njaa huko Darfur, ikiwa ni pamoja na Al Fasher, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini linalozingirwa na wanamgambo wa RSF. Kambi ya Zamzam iliyoko kilomita 12 kutoka Al Fasher, wanakoishi wakimbizi wa ndani pia imekumbwa na hali hiyo.

Hali kama hiyo pia inaweza kuathiri sehemu za Al Fasher na hususan makambi ya Abu Shouk na Al Salam, ingawa idadi ya waathirika na hali ya usalama wa chakula na afya kwenye maeneo yaliyoathirika bado hizijatathminiwa. Kulingana na IPC hali ya njaa katika kambi ya Zamzam ilichochewa na mzozo na vikwazo vikali vilivyozuia misaada ya kiutu kufika kwenye eneo hilo.

Soma zaidi: Amnesty yataka vikwazo vya silaha kote Sudan

Watu wakiwa kwenye foleni ili kujiandikisha kwa ajili ya kupata msaada wa chakula katika kambi ya wakimbizi wa ndani (IDP) huko Agari, Kordofan Kusini, Juni 17, 2024.Picha: Guy Peterson/AFP

Shirika la Early Warning Sytems Network ama FEWS NET liliunga mkono ripoti hiyo ya IPC iliyotolewa siku ya Alhamisi ikisema kuna ushahidi wa kutosha kwamba kulikuwa na njaa katika kambi hiyo ya Zamzam.

Karibu watu milioni 10 wamekimbia makwao kutokana na vita vya Sudan

Karibu watu 320,000 wanaaminika kuwa wameyakimbia makazi yao huko Al-Fasher tangu katikati ya mwezi Aprili limesema IPC na karibu watu 150,000 wanadhaniwa kukimbilia kwenye kambi hiyo hadi mwezi Mei, katika mzozo mbaya kabisa kushuhudiwa ulimwenguni.

Soma pia:Watu milioni 117 wanaishi kama wakimbizi duniani

Wataalamu na maafisa wa Umoja wa Mataifa, wanasema kiwango cha njaa nchini Sudan kinaweza kuchochea hatua zaidi, labda kuanzia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuandaa azimio la kuwezesha mashirika kupeleka misaada kwenye maeneo ya mipaka, sawa na vile walivyofanya nchini Syria, mwaka 2014.

Hata hivyo, azimio kama hilo linaweza kupingwa katika wakati ambapo jeshi la Sudan likiwa tayari limeashiria kupinga kiwango hicho cha njaa kwa hofu ya kupoteza mamlaka ya udhibiti wa mipaka.

Vita nchini Sudan vimeliathiri vibaya taifa hilo kuanzia mji mkuu Khartoum na kuwaweka katika hali ngumu raia, na karibu watu milioni 10.7 wameyakimbia makazi yao, hii ikiwa ni kulingana na Shirika la Kimataifa la Wahamiaji, IOM, miongoni mwao ni milioni 7.9 waliokimbia kutokana na vita vya sasa.

Soma zaidi: Marekani yaandaa mazungumzo ya kusitisha mapigano Sudan

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW