1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya sintofahamu yaendelea kutawala Zimbabwe

16 Novemba 2017

Rais Robert Mugabe amesisitiza kwamba atasalia kuwa mtawala pekee halali wa taifa hilo, kimesema chanzo kimoja cha kijasusi, huku akimkataa Padri Fidelis Mukonori kusimamia mazungumzo ya upatanishi.

BG Mugabe wurde Premierminister 18.04.1980
Picha: picture-alliance/abaca/G. Buthaud

Rais Robert Mugabe amesisitiza kwamba atasalia kuwa mtawala pekee halali wa taifa hilo, kimesema chanzo kimoja cha kijasusi leo hii, huku akimkataa padri wa kanisa Katoliki Fidelis Mukonori kusimamia mazungumzo ya upatanishi yatakayoruhusu mpiganaji huyo wa zamani wa msituni mwenye umri wa miaka 93, kuondoka kwa amani baada ya mapinduzi ya kijeshi. 

Padri huyo, Fidelis Mukonori, atakuwa kama kiunganishi kati ya Rais Mugabe na majenerali wa jeshi, ambao walikamata mamlaka jana Jumatano, katika kile kinachoelezwa kama operesheni dhidi ya "wahalifu" miongoni mwa watu walio ndani ya utawala wake, mwanasiasa mwandamizi ameliambia shirika la habari la Reuters.  

Chanzo hicho hakikufafanua zaidi kuhusu mazungumzo hayo, ambayo yanaonekana yana lengo la kufanikisha hatua ya kukabidhi madaraka kuwa ya amani na kutogubikwa na machafuko baada ya kuondoka kwa Mugabe, ambaye ameliongoza taifa hilo tangu uhuru wake mwaka 1980. 

Ripoti za kijasusi za Zimbabwe zilizoonwa na shirika la habari la Reuters, zinahitimisha kwamba mkuu wa zamani wa usalama wa taifa, Emmerson Mnangagwa, aliyefukuzwa akiwa makamu wa rais mwezi huu, amekuwa akifanya mipango na jeshi na upande wa upinzani kwa zaidi ya mwaka mmoja, ya namna ya kumuondoa Mugabe madarakani. 

Kurejea kwa kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai nako kunaelezwa kama kunachochea minong'ono kwamba mipango hiyo inawezekana itaanza kutekelezeka. Tsvangirai amekuwa nchini Uingereza na Afrika Kusini akipata matibabu ya saratani, na amerejea mjini Harare jana Jumatano, amesema msemaji wa kiongozi huyo

Rais wa Guinnea na mkuu wa Umoja wa Afrika, AU, Alpha Conde, ameitaka Zimbabwe kuitii katiba ya nchiPicha: Getty Images/M. Medina

Umoja wa Afrika waitaka Zimbabwe kuzingatia katiba ya nchi.

Alipozungumza na kituo cha televisheni cha shirika la habari la Ujerumani la DW, pembezoni mwa mkutano unaohusu mabadiliko ya hali ya hewa mjini Bonn, rais wa Guinnea ambaye pia ni mkuu wa Umoja wa Afrika, Alpha Conde kuhusiana na hali ilivyo nchini humo, amesema.

Conde amesema, Umoja wa Afrika haukubaliani na hatua zozote za nguvu za kuangusha serikali. Amesema ametuma ujumbe, akitoa mwito kwa jeshi kurejea kwenye makambi na kuzingatia taratibu za kikatiba. Aidha ameahidi kuwasiliana na rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini atakapowasili Ufaransa, ili kuangalia namna ya kuzungumza moja kwa moja na Rais Mugabe aliyeko katika kizuizi cha nyumbani.

Kuhusiana na iwapo Umoja wa Afrika utajihusisha na usuluhishi wa mzozo huo, Conde amesema hakutakuwa na usuluhishi wowote, na kusisitiza ni lazima jeshi lifuate katiba, ingawa amesema Umoja huo unaweza kukutana na kujadili hatua zaidi iwapo hali itazidi kudorora.

Kiongozi wa upinzani na aliyewahi kuwa waziri wa fedha nchini humo Tendai Biti, ametoa mwito wa kuchaguliwa serikali ya mpito na kuchukua mamlaka. Chama hicho kimesema kwenye taarifa yake kwamba serikali ya mpito inatakiwa kuhusisha Wazimbabwe wenye uwezo ambao majukumu yao yatakuwa ni kuandaa hatua za kubadilisha hali ya uchumi.

Mazungumzo yanaendelea nchini humo ya kutatua mzozo wa kisiasa na kile kinachotajwa kama mwisho wa zama za utawala wa muda mrefu wa rais Robert Mugabe. Maafisa wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, nao wanakutana nchini Botswana kujadili mzozo huo.


Mwandishi: Lilian Mtono./Rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW