1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yaadhimisha siku ya uhuru

9 Julai 2015

Akizungumza katika mkesha wa siku ya uhuru, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema matumaini ya nchi hiyo wakati ilipopata uhuru yamegeuka na kuwa hali ya kukata tamaa.

Südsudan Feierlichkeiten Unabhängigkeit
Picha: CHARLES LOMODONG/AFP/Getty Images

Ban amesema hali ya Sudan Kusini ni ya kukatisha tamaaa kwa sababu taifa hilo changa kabisa duniani limegubikwa na mgogoro wenye “viwango vikubwa kabisa vya machafuko na matukio yasiyokubalika ya udhalilishaji kingono”.

Ametoa wito kwa Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar “kudhihirisha uongozi wao” kwa kutafuta suluhisho la kisiasa na kukamilisha maramoja makubaliano ya amani. Aidha amesema jamii ya kimataifa lazima ichukue hatua muhimu za kusaidia kumaliza mapigano.

Kiir ametawazwa jana kama Rais wa Sudan Kusini kwa miaka mingine mitatu baada ya bunge kuahirisha uchaguzi na kuurefusha muhula wake kutokana na mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Bunge liliamua kuwa Kiir hakustahili kuapishwa rami kwa sababu tayari alikuwa madarakani. Rais Kiir aliliahidi bunge kuwa “atahakikisha amani” na “maridhiano” na kiongozi wa waasi Riek Machar.

Kiongozi wa waasi Riek Machar na Rais Salva Kiir wameshindwa kufikia suluhisho la amaniPicha: Getty Images/Zacharias Abubeker/Ashraf Shazly/Montage

Lakini Machar ameonya juu ya kuzuka upya mapigano ikiwa Rais Salva Kiir ataendelea kuwa madarakani. Akizungumza mjini Nairobi, Machar amesema muhula huo mpya wa miaka mitatu kwa Rais Salva Kiir sio halali

Naye Mkuu wa shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa Herve Ladsous amelishinikiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana kuiwekea Sudan Kusini vikwazo vya silaha pamoja na kuwawekea vikwazo viongozi zaidi wa pande zote hasimu katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita. Wiki iliyopita baraza hilo liliwawekea vikwazo majenerali sita wa Sudan Kusini, watu wa kwanza ambao mali zao zimezuiwa na kupigwa marufuku kusafiri ng'ambo.

Wanadiplomasia wanasema baraza la usalama halikukubaliana kuhusu kutangaza vikwazo vya silaha wakati lilipounda kamati ya vikwazo mwezi Machi, ambapo Marekani, Urusi na China zilipinga wakati Ulaya na wanachama wengine wa baraza hilo wakiunga mkono. Badala yake, baraza la usalama lilitishia tu kuchukua hatua ya aina hiyo.

Ladsous amesema inasikitisha kuwa viongozi hao wawili wamesaini zaidi ya mikataba saba ya kusitisha mapigano lakini hakuna hata mmoja uliotekelezwa ili kuweka matumaini ya suluhisho la kisiasa. Ameongeza kuwa kuna uwezekano uhalifu dhidi ya ubinaadamu na uhalifu wa kivita umefanyika nchini humo na wanaohusika wanastahili kuwajibishwa.

Vita vya kikabila kati ya wadinka kabila atokealo Kiir na wanuer kabila la Machar vimeligawa jeshi la nchi hiyo na kusababisha mzozo mkubwa nchini humo ambao umepelekea maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuachwa bila ya makaazi.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW