Hali ya uhuru wa vyombo vya habari Zimbabwe
1 Julai 2005Wandishi wa habari wa Zimbabwe wanajaribu kufanya kazi katika mazingira magumu. Conrad Dube, anafanya kazi katika Gazeti la ‘Zimbabwe Independent’. Gazeti hili linalochapishwa kila wiki linamilikiwa na kampuni binafsi. Anasema, nchini Zimbabwe hamna udhibiti rasmi wa vyombo vya habari, lakini atakaye kosoa serikali ategemee kwamba polisi au vikosi vya usalama vitamfuatilia. Bwana Dube anaeleza:
“Wandishi wa habari wetu wengi wamekamatwa au wamefunguliwa mashtaka, lakini cha kushangaza ni hamna aliyehukumiwa kwa sheria za sasa hivi, kwa sababu Mahakama Kuu na Mahakama nyingine zimesema haziwezi kutekeleza sheria hizo sababu zinapingana na katiba ya nchi. Mtu ana uhuru wa kuandika, lakini baada ya kuandika anapoteza uhuru wake”.
Wazimbabwe wanadhani ni vigumu kwa sasa kupata habari zinazoaminika kupitia vyombo vya habari vya kila siku, ndio maana wanaenda kwenye mtandao. Kwenye mtandao wanaweza kusoma habari zilizoandikwa na wandishi wa habari wanaoishi Afrika Kusini au Ulaya, wanaopata maelezo yao kutoka kwa wenzao walio Zimbabwe.
Hata Chengetai Muriwa anaandika habari zake kwenye mtandao. Alikuwa anafanya kazi kwenye gazeti la ‘Daily News’ lililokuwa linamilikiwa na kampuni binfasi, lakini sasa tangu miaka miwili sasa limepigwa marufuku. Kwa sababu gazeti hilo haliruhusiwi kuchapishwa, naye Bwana Muriwa haruhusiwi kufanya kazi kama mwandishi wa habari. Lakini na yeye pia huwa anatafuta habari zisizotoka serikalini.
Bwana Muriwa anasema:
“Unaweza ukawa na wanaotaka kukupa maelezo juu ya maovu yanayofanywa na serikali. Wanakupa maelezo hayo kwa siri. Sasa kwa upande wangu, naandika habari hiyo na kuituma kwenye mtandao, lakini sitaji walionipa maelezo. Pia siandiki jina langu kama mwandishi wa habari hiyo, maana nitakamatwa”.
Mojawapo ya mada anazozifuatilia ni kuhusu kuvunjwa kwa nyumba za watu mijini. Tangu mwisho wa mezi Mei, utawala wa Rais Mugabe umewafanya watu 400,000 wakose makazi, kwa sababu ya kusitisha ujenzi ovyo usiofuata mpango uliowekwa. Bwana Dube anadhani kwamba sababu hii haitoshi kwa sababu hali hii ilisababishwa na serikali yenyewe. Bwana Bude anaeleza zaidi:
“Wametawala kwa miaka 20, watu walianza kujenga tangu miaka 20 iliyopita, wakati uongozi huu ukitawala na halmashauri za miji zikawaachilia wajenge. Vyama vya ushirika vingi viliyokuwa vikijenga katika miji, vinaungwa mkono na chama cha siasa cha ZANUF PF, kwa sababu vinaongozwa na askari wastaafu, walipigania uhuru. Kinachoshangaza ni serikali wanageuka na kusema wanataka kusafisha miji, wakati wao ndio walio achilia ujenzi uendelee”.
Kwa maoni ya Bwana Dube kwa sababu Rais Mugabe anawaadhibu wale wanaomkosoa, basi msimamo wa Jumuiya ya Kimtaifa ni muhimu, haswa ule wa nchi jirani za Afrika. Kwa maoni ya Bwana Dube:
Kinacho vunja moyo ni viongozi wengi wa Afrika wana unga mkono chama tawala cha ZANUF PF na Rais Mugabe, wanafanya hivyo kwa madai kwamba yeye ni mwafrika mwenzao. Hawampingi hadharani, haswa Afrika Kusini”.
Siku chache zilizopita, zaidi ya mashirika 200 ya kutetea haki za binadamu, mengi yamashirkia hayo kutoka Afrika, waliuomba Umoja wa Afrika uchukue hatua. Bwana Dube anaona hii itaweza kuzisaidia vyama vya kutetea haki za raia nchini Zimbabwe. Anasema katika mkutano uliopita wa Umoja wa Afrika, baadhi ya mashirika hayo kutoka Zimbabwe, yalijaribu kuingiza suala la nchi yao kwenye ajenda, wakashindwa.
Kwa maoni ya Bwana Dube, mashirika hayo yangeweza kuungana na kuzungumza kwa sauti moja, labda wangefanikiwa. Na kwenye mkutano wa Umoja wa Afrika wangejadili na kuchunguza matukio yanayoendelea Zimbabwe.