Hali ya usalama yazorota Guinea
17 Novemba 2010Marekani nayo imejiunga na jumuiya ya kimataifa kuwataka wapinzani wakubwa wa kisiasa nchini Guinea wamalize tafauti zao kwa njia za kisheria na kidiplomasia, badala ya kuwaachia wafuasi wao kushambuliana.
Hapo jana (16 Novemba 2010), msemaji wa Mambo ya Nje wa Marekani, Philip Crowley, aliwatolea wito mtu aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi wa marudio Alpha Conde na mpinzani wake Cellou Dalein Diallo wainusuru Guinea isitumbukie tena kwenye machafuko.
"Tunaelewa kuwa mgombea wa upinzani Cellou Diallo anapanga kuyapinga matokeo ya uchaguzi mahakamani na tunamuomba Bwana Diallo atumie njia za kisheria na apeleke malalamiko yake kwenye Mahakama Kuu." Amesema Cowley.
Juzi (15 Novemba 2010), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, aliwataka raia wa Guinea wakubaliane na matokeo ya uchaguzi huu na kumaliza tafauti zao kwa njia za amani. Katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Ban Ki-moon aliwataka raia wa Guinea "kwa maslahi ya taifa lao, wakubali matokeo ya uchaguzi na watatue tafauti zao kwa njia za kisheria."
Tume Huru ya Uchaguzi ilimtangaza kiongozi wa upinzani, mwenye miaka 72, Alpha Conde, kuwa ni mshindi wa uchaguzi wa marudio, akiwa amepata asilimia 52.52, akimshinda Diallo aliyepata asilimia 47.48. Lakini chama cha Diallo, Union of Democratic Forces of Guinea, UFDG, kiliyapinga vikali matokeo hayo, kikidai kwamba yamepikwa na kwamba wafuasi wake waliteswa na utawala wa kijeshi katika upigaji kura na utangazaji wa matokeo.
Mashahidi wanasema kwamba milio ya risasi ilianza kusikika kutoka maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Conakry mara baada ya matokeo hayo kutangazwa, pale wafuasi wa Diallo walipoanza kuingia barabarani kuyapinga. Imeripotiwa kwamba hadi sasa tayari watu wanne wameshafariki dunia kutokana na machafuko yaliyotokana na utangazaji wa matokeo hayo hapo juzi.
Hadi sasa watu wanne wameshafariki dunia na zaidi ya darzeni kujeruhiwa kutokana na machafuko haya na kuna uwezekano wa vifo na majeruhi wengine, kwani hali bado haijawa shuwari.
Uchaguzi huu ulikusudiwa kumaliza utawala wa kijeshi ambao ulichukua madaraka mwaka 2008 baada ya kifo cha Lansana Conte aliyeongoza nchi hiyo masikini ya Afrika ya Magharibi kwa zaidi ya miongo miwili.
Mshindi wa uchaguzi huu, Alpha Conde, anasifika kwa kuwa kwenye upinzani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika. Alikaa kwenye upinzani kwa miaka 50 kabla ya juzi kutangazwa mshindi wa urais.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miiraji