1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya vyombo vya habari Rwanda

Lillian Urio23 Agosti 2005

Baadhi ya vyombo vya habari vya Rwanda vilihusika na mauaji ya halaiki yaliotokea mwaka 1994 kwa kurusha matangazo yaliochochea mauaji hayo. Je leo hii hali halisi ya vyombo vya habari nchini humo ikoje?

Radio ya kibinafsi ya ‘Radio des Mille Collines’ ilikuwa ikimilikiwa na baadhi ya maafisa wakuu serikalini wenye siasa kali za ubaguzi wa kikabila. Radio hiyo ilichochea mauaji ya halaiki nchini Rwanda.

Ingawa kulikuwa na wanandishi wa habari waliochangia katika mauaji wengine wengi walikuwa wahanga. Wandishi wa habari 70 waliuwawa katika kipindi hicho.

Leo hii Rwanda ina katiba mpya na tangu mwaka 2002 kuna sheria mpya ya vyombo vya habari, ambayo inawapa wandishi wa habari uhuru wa kufanya kazi yao.

Miaka 11 baada ya tukio hilo la kusikitisha Rwanda ni nchi ya amani. Lakini je, vyombo vya habari vina nafasi gani katika jamii na vinatekelezaje kazi zao?

Radio ni muhimu sana nchini humo sababu karibu asilimia 41 ya nyumba zina radio. Hivyo ni rahisi kuwafikishia wananchi ujumbe ukilinganisha na asilimia 0.1 ya nyumba zenye televisheni. Pia sehemu kubwa ya nchi ina tatizo la ukosefu wa umeme na hamna gazeti linachapishwa kila siku, lakini yapo magazeti 16 yanaotoka kila wiki au mwezi.

Bwana Joseph Bideri, Mkurugenzi wa Radio ya taifa, alipoulizwa kama radio yake inaikosoa serikali alitoa mfano wa kipindi cha ‘townmeeting’. Kipindi hicho kinarushwa moja kwa moja kila wikiendi na mgeni anakuwa mwanasiasa na wannchi wanapiga simu na kumuuliza mwanasiasa huyo maswali.

“Tunachofanya ni kupokea simu na wanasiasa wanajibu maswali. Hatuchagui nani apige simu. Watu wanapiga simu za mkono wakiwa kwenye magari yao, wengine kutoka kwenye simu za mitaani. Kipindi kinapendwa sana.”

Mada za vipindi vijavyo zinatajwa kabla. Lakini mada nzito kama rushwa hazizungumziwi.

Pamoja na kuwepo na radio na televisheni za taifa, pia kuna vymbo vingine vya habari 10 vya kibinafsi, vikiwemo Radio Dix, Radio Flash, Radio Maria na Radio Contact FM.

Vyombo hivyo vingependa kutumika kama vigezo vya kuonyesha jinsi vyombo vya habari nchini vina uhuru. Lakini mwandishi wa habari, Furaha Mugisha, anakosoa radio zinazomilikiwa na watu binafsi.

“Wanacheza muziki na kuwaburudisha watu. Lakini hawawezi kuwa na vipindi vyenye mada nzito, kama vile masuala ya siasa au yatakayo wagusa viongozi wa ngazi za juu. Kwa hivyo, ingawa inasemekana vyombo vya habari vina uhuru, lakini hawana uhuru kikamilifu.”

Bwana Mugisha anafanya kazi katika gazeti la ‘Umuseso’ ambalo mara kwa mara linakosoa serikali ya Rwanda. Gazeti hilo limekuwa na migogoro na baadhi ya viongozi wa serikalini hadi mbunge mmoja aliwahi kumfungulia mashataka mhariri mkuu wa ‘Umuseso’.

Waziri wa Habari, Laurent Nkusi, anapinga kwamba serikali inajiingiza katika shughuli za wandishi wa habari.

“Hatuingilii kazi zao. Tunakubali kukosolewa. Lakini tukiona kwamba ripoti zinaweza kuharibu umoja wa Rwanda au kuna chombo cha habari kinachoelekea kuwa na sera za siasa kali, kama ilivyotokea hapo awali, basi tunaingilia. Lakini hadi sasa kuna gazeti moja tu ‘Umuseso’ lililofikishwa mahakamani, kutokana na matatizo kati yao na mbunge. Hata hivyo hatujalipiga marufuku gazeti hilo.”

Miaka miwili iliyopita baraza la vyombo vya habari lilianzishwa, lenye wanachama kutoka mashirika ya kibinafsi, serikali na vikundi vya kijamii. Pamoja na kuwa na jukumu la kutoa leseni Baraza hilo pia lina angalia aina za habari zinazotolewa na vyombo vya habari nchini na linaingilia kati pale mwandishi wa habari anaponyanyaswa.

Sheria za kazi zipo lakini wakati mwingine zina kuwa na vizingiti hasa pale mwanandishi wa habari anapotaka kufanya upelelezi juu ya habari fulani. Pia malipo ya wandishi wa habari sio mazuri na inabidi wafanye shughuli nyingine ili waweze kumudu maisha.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW