Hali ya wanasiasa wa Ethiopia yazidi kudorora magerezani
25 Februari 2021Wakili Tokuma Daba aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba wanne kati yao wameendelea na mgomo wao wa kutokula na afya yao inazorota haraka, na kuongeza kwamba aliwatembelea mara ya mwisho siku ya Jumatatu.
"Wasiwasi wetu ni juu ya maisha yao. Tunaambiwa na madaktari kwamba wanahitaji matibabu magumu ya kiafya, ambayo hayapo sasa hivi. Ni jambo linalotia wasiwasi kweli."
Wanasiasa hao waliofungwa ni pamoja na mmiliki wa vyombo vya habari aliegeuka mwanasiasa Jawar Mohammed, Bekele Gerba, Hamza Adane na Dejene Tafa.
Soma zaidi: Mahusiano ya Ujerumani-Ethiopia yayumba kuhusu Tigray
Walikamatwa pamoja na wengine wasiopungua 16 kufutia mauaji ya mwanamuzi maarugu, Hachalu Hundessa, mnamo Juni 2020.
Kufuatia hasira juu ya mauaji hayo, vurugu zinazowalenga watu wa jamii za wachache zilisababisha vifo vya watu kadhaa, wengi wao kutoka mkoa wa Oromia.
Baadhi ya watu wa jamii ya Oromo wanahisi kiu yao ya demokrasia na uhuru wa kuchagua viongozi wao haijatimizwa tangu waziri mkuu Abiy Ahmed alipoingia madarakani mwaka 2018.
Wanamtuhumu kuvunja baadhi ya ahadi zake kwa kuwakamata baadhi ya wanasiasa waliorejea Ethiopia kutoka nje, akiwemo Jawar, baada ya kuingia madarakani.
Soma pia: UN: Hali ya Ethiopia inahitaji uangalizi wa dharura
Wanasiasa waliofungwa wanakabiliwa na mashtaka yakiwemo kula njama kusambaratisha katiba kwa mbavu na makosa mengine yanayohusiana na ugaidi. Wanakanusha mashtaka hayo wanayodai yanachochewa kisiasa.
Wito wa kubadili mwelekeo
Namna wafungwa hao "wanavyotendewa na serikali Ethiopia inapalilia mzozo mzito, hasa wakati ambapo afya yao inazidi kuzorota," balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa na sasa mteule wa rais Joe Biden kwa nafasi ya mkuu wa misaada ya kigeni wa nchi hiyo Samantha Power alitweet wiki iliyopita, akisema ni muhimu kwa serikali "kubadili mwelekeo kabla haijachelewa."
Wafungwa hao wanadai kukamatwa kwao kunalenga kuwanyima fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu ujao nchini Ethiopia mwezi Juni. Siku ya Jumanne, bodi ya uchaguzi ya Ethiopia ilibainisha wazi kwamba wanasiasa walioko korokoroni hawataweza kujiandikisha kama wagombea.
Soma pia: Kamatakamata Ethiopia yaibua hofu ya ukandamizaji wa zamani
Tokuma alisema wateja wake wanafanya mgomo wa kula kwa sababu kadhaa ikiwemo kupinga unyanyasaji na kukamatwa kwa wafuasi wao na wanafamilia.
Wateja wake pia wanataka kuachiwa kwa wafungwa wote wa kisiasa. Wafungwa hao wanaogoma wamekataa kutibiwa katika hospitali za serikali, wakipendelea za kibinafsi.
Wiki iliyopita balozi wa Ethiopia nchini Marekani, Fitsum Arega, alisema katika ujumbe wa Twitter kwamba pendekezo la kuwatibu kwenye hospitali ya kijeshi yenye hadhi sawa na ile ya Walter Reed nchini Marekani bado linasimama.
Jumanne mahakama ya juu ya Ethiopia iliamuru wafungwa hao wapatiwe matibabu kutoka hospitali binafsi, lakini matibabu yanapaswa kufanyika ndani ya gereza la Kaliti wanakoshikiliwa.
Soma pia: Watu 240 wauawa Ethiopia
Henok Gabissa, rais wa zamani wa chama cha utafiti cha Oromo na mwangalizi wa siasa za Ethiopia alisema hali katika mkoa wa Oromia ni mbaya, na kuongeza kwamba utawala wa Abiy unawazuwia wanasiasa wa Oromo.
"Vyama vya upinzani vya Oromo vina uhalali zaidi kuliko uatawala wa Abiy. Umma katika mkoa huo unawaunga mkono wafungwa na madai yao," alisema.
Katika chapisho la mtandao wa kijamii siku ya Jumatano, Abiy alisema "jukumu la wazi la serikali ni kuhakikisha kwamba uchaguzi wa amani, huru na wa haki unafanyika katika duru hii inayosubiriwa pakubwa." Aliongeza, "tumeweka msitari wa kutochanganya kazi za chama na serikali."
Baadhi ya vyama vya siasa nchini Ethiopia tayari vinadai kukabiliwa na ugumu katika kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi kama vile unyanyasaji, kamatakamata na hata mauaji ya baadhi ya wanachama wao.