1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya wanawake nchini Saudi-Arabia

Reinhard Baumgarten / Maja Dreyer15 Machi 2006

Wanawake nchini Saudi-Arabia wanaishi maisha ya kujificha. Wanakaa ndani, wanajifunga kabisa, wanawekwa kando ya jamii. Lakini hali nchini humo inabadilika. Katika vita vigumu vya kupigania uhuru wao, wanawake wa Saudi-Arabia wanatafuta njia ya kujiukomboa.

Wanawake nchini Saudi-Arabia wanataka kujikomboa
Wanawake nchini Saudi-Arabia wanataka kujikomboaPicha: AP

Wakitembea nje wa nyumba zao, wanawake nchini Saudi-Arabia kwa kawaida wanavaa mabuibui meusi. Hawaruhusiwi kupiga kura, hawawezi kusafiri bila ya ruhusa maalum, na hawaruhusiwi kuendesha gari.

Lakini hali yao inaendelea kuwa afadhali kidogo, anasema mwandishi wa habari Afaf el-Abdullah: “Maisha yao ni bora kuliko zamani. Hata tayari wanashindana na wanaume, kwa mfano, katika uchaguzi wa baraza la wafanyabiashara. Haya hayakuwepo mpaka juzi.”

Suhila Hammad, lakini, ambaye ni mhamasishaji mtendaji wa haki za binadamu na wanawake nchini Saudi-Arabia ana maoni mengine. Anaeleza: “Mwanamke wa Kisaudi yuko kati kati baina ya maji kupwa na maji kujaa. Anaendelea mbele kwa hatua ndogo ndogo, anapigania haki zake, lakini halafu wengine wanakuja na wanamfuta tena arudi nyuma. Sisi tunasumbuliwa, mimi ninasumbuliwa. Nikianza mjadala na wasomi, wanauliza mbona unathubutu kumchokoza msomi ambaye ana mamlaka makubwa juu ya wanawake? Basi, nijibu nini?”

Lazima Saudi-Arabia ibadilike, anasema Bibi Suhila. Ufalme huo unakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii. Mfano mmoja ni idadi ya watu wasio na ajira inazidi kuongezeka. Karibu asilimia 30 ya wanaume vijana wa nchi hiyo hawana ajira. Kwa upande wa wanawake idadi ni kubwa zaidi.

Asilimia 7 tu ya wanawake wana kazi ya kupata mshahara, ingawa naibu waziri wa habari, Saleh al Namlah, anasisitiza kuwa wanawake wengi wanafanya kazi: “Wanawake wa Kisaudia wanaingia katika kila kazi, hasa katika elimu. Lakini pia siku hizi kuna wafanyabiashara wa kike. Katika benki, wanawake wengi wamepata vyeo vya juu.”

Mhamasishaji wa haki za wanawake, Bibi Suhila Hammad, anasema haya ni mambo yasoyofuata kawaida. Hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kuwakatalia asilimia 50 ya wananchi wake haki zao za kimsingi. Anasema: “Wanawake ndio changamoto kubwa zaidi kwa nchi zote za Kiarabu na Kiislamu. Wanaanza kupigania haki zao kila pahali. Wanasema: tupe haki zetu kufuata dini yetu. Nchi za Kiislamu haziwezi kuendelea ikiwa hali ya wanawake inabaki kama ilivyo hivi sasa.”

Maoni haya yanaungwa mkono na ripoti maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo ya binadamu katika nchi za Kiarabu. Lakini uchunguzi huo hausikilizwi na viongozi kiume!

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW