Hamas haitashiriki mazungumzo ya kusimamisha vita
14 Agosti 2024Uamuzi huo unatatiza kufikiwa hatua ya kuleta suluhu ambayo Iran imesema ingeliizuia kuishambulia Israel, ili ulipiza kisasi kifo cha kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh aliyeuliwa mjini Tehran hivi karibuni.
Hata hivyo Marekani inatarajia mazungumzo, ambayo si ya ana kwa ana yatafanyika, mjini Doha kama ilivyopangwa.
Israel imesema itapeleka ujumbe mjini Doha lakini Hamas imeeleza kuwa inataka uwepo mpango wa kulitekeleza pendekezo ambalo imeshalikubali, badala ya kushiriki kwenye mazungumzo zaidi.
Wakati huo huo tovuti ya Axios ya nchini Marekani imeripoti kwamba waziri wa mambo nje wa Marekani Antony Blinken ameahirisha ziara ya Mashariki ya Kati iliyokuwa ianze jana Jumanne.
Israel yashutumiwa kuwanyanyasa Wapalestina walio gerezani
Kwengineko Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas anatarajiwa kukutana na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwenye ikulu mjini Ankara, siku moja baada ya kufanya ziara nchini Urusi.
Abbas anafanya ziara hiyo katika muktadha wa mvutano mkubwa kutokana na vita vya miezi 10 kati ya Hamas na Israel na pia kutokana na kushindikana kwa juhudi za kusimamisha mapigano na kitisho cha Iran kuishambulia Israel.
Rais huyo wa mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas, pia atalihutubia bunge la Uturuki katika kikao maalum kuhusu suala la Palestina hapo kesho Alhamisi.