1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas: Tumejitolea kutekeleza makubaliano ya amani

17 Oktoba 2025

Kundi la wanamgambo la Hamas limesema limejitolea kutekeleza makubaliano ya amani yaliosimamiwa na Marekani yaliositisha vita vyake na Israel, na kurejesha miili yote ya mateka ambao bado hawajulikani walipo.

Mama ya mateka wa Israel Idan Shtivi, ambaye mwili wake ulirejeshwa na jeshi la Israel baada ya kutekwa na kuuawa na Hamas, aomboleza katika kaburi lake mnamo Septemba 1, 2025
Familia za mateka wa Israel Picha: Yael Guisky Abas/SOPA Images/ZUMA/picture alliance

Hamas imesisitiza nia yake ya kukabidhi maiti zote zilizosalia za mateka wa Israel lakini imesema mchakato huo huenda ukahitaji muda zaidi kwani baadhi ya maiti hizo zilizikwa chini ya vifusi vya majengo yalioharibiwa na mashambulizi katika eneo hilo.

Ikiitikia wito wa kundi hilo la wanamgambo wa kutaka usaidizi wa kutafuta miili ya mateka 19 waliofukiwa chini ya vifusi pamoja na idadi isiyojulikana ya Wapalestina, Uturuki imetuma wataalamu kusaidia katika shughuli hiyo ya utafutaji.

Uturuki imetuma makumi ya wataalam wa misaada ya majanga kusaidia kutafuta miili hiyo, lakini familia za mateka wa Israeli waliouawa, zimekasirishwa na kushindwa kwa Hamas kutoa mabaki ya wapendwa wao.

Trump atoa wito wa subra katika kurejeshwa kwa mateka wa Israel

Rais wa Marekani Donald Trump, ameonekana kutoa wito wa subira linapokuja suala la kurejeshwa kwa miili hiyo akisisitiza kuwa Hamas inatafuta mabaki ya mateka, lakini baadaye alionyesha kughadhabishwa na mwenendo wa kundi hilo tangu kusitishwa kwa mapigano.

Kupitia ujumbe kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema ikiwa Hamas itaendelea kuwauwa watu Gaza ambayo sio makubaliano, hawatakuwa na chaguo ila kuwauwa katika kile kilichoonekana kumaanisha mauaji ya hivi karibuni ya raia wa Palestina.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: Alex Kolomoisky/REUTERS

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, alisisitiza tena azma yake ya kuhakikisha kurejeshwa kwa mateka wote baada ya waziri wake wa ulinzi kuonya kwamba jeshi litaanzisha tena mapigano ikiwa Hamas itashindwa kufanya hivyo.

Malori ya misaada yaondoka Rafah

Malori ya mafuta na bidhaa za misaada ya kuelekea Gaza, yameonekana leo yakitoka katika eneo la mpaka wa Rafah nchini Misri.

Hapo jana, waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Sa'ar alinukuliwa na shirika la habari la Italia ANSA akisema kwamba kivuko hicho cha Rafah kilichoko kati ya Gaza na Misri huenda kitafunguliwa tena siku ya Jumapili.

Hata hivyo hakufafanua ikiwa kivuko hicho kitafunguliwa kwa ajili ya kupitisha misaada ya kibinadamu, au kwa ajili ya watu.

Iran yashtumu mashambulizi ya Israel nchini Lebanon

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmaeil Baqaei, amesema mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon ni ukiukaji wa wazi wa uhuru na uadilifu wa Lebanon.

Hapo jana, Lebanon ilisema kuwa Israel ilimuuwa mtu mmoja na kuwajeruhi wengine saba huku jeshi hilo la Israel likisema kuwa lilikuwa limelilenga kundi la Hezbollah na washirika wake.

    

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW