1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Hamas yamlaumu Waziri Mkuu Netanyahu kwa kukataa amani

23 Agosti 2024

Hamas imemlaumu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa kukataa kufikia mapatano ya kusimamisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Hamas yamkosoa Benjamin Netanyahu kwa kuyakataa makubaliano ya kusitisha mapiganoPicha: Jose Luis Magana/AP Photo/picture alliance

Hamas imemlaumu Netanyahu kwa kuja na madai mapya ya kutaka jeshi la Israel ndilo lipewe udhibiti usio ukomo wa mpaka kati ya Ukanda huo na Misri.

Msemaji wa Netanyahu ameeleza kuwa tayari ujumbe wa Israel upo nchini Misri kuzungumzia juu ya kusimamisha mapigano na kuachiwa kwa mateka. Hata hivyo, wawakilishi wa Hamas hawashiriki.

Misri, Marekani na Qatar zimekuwa zinajaribu kuendeleza mazungumzo tangu kuanza kwa mgogoro zaidi ya miezi 10 iliyopita ili kuvimaliza vita kati ya Israel na Hamas kwenye Ukanda wa Gaza.

Umoja wa Mataifa umesema maelfu ya raia wa Palestina wamelazimika kuondoka tena kutoka mji wa Deir el Balah na mji wa Khan Yunis baada ya jeshi la Israel kuwataka kufanya hivyo.