Hamas yaashiria kuwa tayari kusitisha mapigano
29 Aprili 2024Ujumbe wa Hamas uliwasili mjini Kairo siku ya Jumatatu (Aprili 29), ambako ulitazamiwa kutoa majibu yake kwa pendekezo la hivi karibuni la Israel la makubaliano ya kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka baada ya takribani miezi saba ya vita.
Misri, Qatar na Marekani zimekuwa zikijaribu kuwa wapatanishi kati ya Israel na Hamas kwa miezi kadhaa sasa, lakini katika siku za karibuni shinikizo kubwa zaidi la kimataifa kutaka usitishwaji huo wa mapigano.
Soma zaidi: Blinken aendeleza juhudi za suluhu ya vita vya Israel na Hamas
Kituo cha televisheni cha Al-Qahira News, ambacho kina mafunganamo na idara ya ujasusi ya Misri, kilisema mazungumzo yangelifanyika Jumatatu mjini Kairo, ingawa hakikuweka wazi muda na mahala pa kufanyika.
Hamas yaashiria kukubali mpango wa kusitisha mapigano
Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Hamas alisema siku ya Jumapili (Aprili 28) kwamba kundi hilo "halikuwa na matatizo makubwa sana" na mpango wa kusitisha mapigano uliopendekezwa na Israel.
"Mazingira ni mazuri isipokuwa kuwe na vizuizi vipya kutoka Israel." Afisa huyo aliliambia shirika la habari la AFP.
Soma zaidi: Saudi Arabia yasema vita vya Gaza vinaweza kusababisha athari kubwa kiuchumi duniani.
Chanzo chengine kinachofahamu yanayoendelea kwenye mazungumzo hayo kiliiambia AFP kwamba wapatanishi kutoka Qatar walikuwa nashiriki kwenye mazungumzo hayo ya Kairo, licha ya hivi karibuni Doha kusema kuwa ingelifikiria upya jukumu lake kwenye mazungumzo hayo.
Wakati Israel imeapa kwamba itaendelea na mashambulizi yake ya ardhini kwenye mji wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wa Rafah, licha ya ukosoaji wa kimataifa dhidi ya operesheni hiyo, Waziri wa Mambo ya Kigeni, Israel Katz, alisema kwamba serikali yake inaweza kusitisha uvamizi huo ikiwa makubaliano yatafikiwa.
Blinken akutana na mataifa ya Ghuba
Kwa upande mwengine, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken, aliwasili nchini Saudi Arabua kuhudhuria mkutano wa pamoja kati ya nchi yake na mataifa wanachama wa Baraza la Ghuba mjini Riyadh.
Blinken alisema Marekani ilikuwa inaona "hatua kubwa zimepigwa kwenye hali ya kibinaadamu katika Ukanda wa Gaza" katika wiki za hivi karibuni, ingawa alionya kuwa Israel ilikuwa inapaswa kufanya mengi zaidi kuhakikisha raia wengi zaidi wanafikiwa na misaada na huduma wanazohitaji.
Soma zaidi: Hamas inatathmini pendekezo jipya la Israel la kusitisha mapigano
Blinken aliuambia mkutano huo kwamba njia bora zaidi ya kukomesha hali mbaya ya kibinaadamu iliyopo Gaza ni kusitisha mapigano na kwamba Washington inaendeleza juhudi za kuvizuwia vita vya Gaza visisambae zaidi.
Mwenyeji wa mkutano huo, Waziri wa Mambo wa Kigeni wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan, alisema siku ya Jumapili kwamba "mfumo wa kisiasa wa kimataifa umeshindwa kwenye namna unavyolishughulikia janga la Gaza."
"Suluhisho la kipekee na la kudumu ni kuundwa kwa taifa huru la Palestina ili haya yasijirudie tena," alisema Farhan.
Mkutano huo wa Riyadh uliowajumuisha pia mawaziri wa kigeni wa mataifa ya Ulaya ulidhamiria kutoa msukumo zaidi wa kupatikana makubaliano ya kusitisha mapigano na kuongeza misaada ya kibinaadamu kwenye Ukanda wa Gaza.
Vyanzo: Reuters, AFP