Hamas yakataa kujiunga na serikali
4 Julai 2005Gaza:
Chama cha Waislamu wenye itikadi kali, Hamas, leo kimepuza mwaliko wa kujiunga na Baraza la Mawaziri la Palestina. Rais Mahmoud Abbas wa Palestina anataka kuunda serikali ya umoja wa taifa itakayosaidia kuidhibiti Gaza baada ya Waisraeli kuondoka. Rais Abbas, akikabiliwa na shinikizo la Umma la kupambana na hali ya kutokuwa na sheria katika maeneo ya Wapalestina, juma lililopita ameviomba vikundi vyenye silaha kujiunga na serikali yake ili zoezi la kuwataka Walowezi wa Kiyahudi waondoke katika maeneo ya Wapalestina lifanikiwe. Zoezi hilo litaanza mwezi ujao. Msemaji wa Hamas, Mushir al-Masri amesema kuwa huu siyo wakati wa muwafaka wa kuunda serikali ya umoja wa taifa. Kikundi kingine cha Kiislamu, Jihad, ambacho hakina wafuasi wengi kuliko Hamas, kimelikataa pendekezo hilo moja kwa moja.