1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Hamas yakubali rasimu ya makubaliano ya kusitisha vita Gaza

15 Januari 2025

Kundi la Hamas limekubali rasimu ya makubaliano ya kusitisha vita katika ukanda wa Gaza na kuachiliwa huru kwa mateka. Hayo yameelezwa na maafisa wawili wanaohusika katika mazungumzo hayo yanayofanyika mjini Doha, Qatar.

Gaza | Khan Yunis | Hamas
Wapalestina wakiwabeba watu waliojeruhiwa kuwapeleka hospitali kufuatia shambulio la anga la Israel kwenye jengo la makazi mjini Khan Younes.Picha: Saher Alghorra/Middle East images/AFP/Getty Images

Wapatanishi wa Marekani na mataifa ya Kiarabu wamesema Israel na kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas wako karibu kufikia makubaliano, hatua ambayo itaashiria kuvimaliza vita vilivyodumu zaidi ya miezi 15.

Shirika la Habari la Associated Press limepata nakala ya makubaliano yaliyopendekezwa ya kusitisha mapigano, huku maafisa wa Misri na Hamas wakithibitisha uhalali wa nakala hiyo.

Soma pia: Vyanzo: Mkataba usitishaji wa vita Gaza unakaribia 

Afisa wa Israel amefahamisha kuwa maendeleo makubwa kuelekea kufikia makubaliano hayo yamepatikana, japo maelezo ya mwisho bado yanafanyiwa kazi. Maafisa hao wote watatu - wa Misri, Hamas na Israel, wamezungumza kwa sharti la kutotajwa majina.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, anaamini kuwa wanakaribia kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kuongeza kwamba, uamuzi huo uko mikononi mwa Hamas.

Amesema, "Tuko karibu sana. Karibu zaidi kuliko wakati wowote ule, taarifa rasmi inaweza kutolewa aidha ndani ya saa chache au masiku.”

Wapalestina wakiomboleza vifo vya jamaa zao waliouawa kufuatia shambulio la Israeli lililolenga gari lililobeba waandishi wa habari.Picha: Naaman Omar/APA/ ZUMA/picture alliance

Marekani, Misri na Qatar zimekuwa katika mstari wa mbele kuongoza juhudi za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka.

Inaripotiwa kwamba takriban watu 100 bado wanashikiliwa mateka ndani ya Gaza, huku jeshi la Israel likiamini kuwa watu wapatao 33 tayari wamekufa.

Soma pia: Shirika la Msalaba Mwekundu latoa wito wa dharura Gaza 

Makubaliano yoyote yatakayofikiwa yanatarajiwa kusitisha mapigano na kufungua fursa ya matumaini ya kupunguza vita vikali na vya na uharibifu ambavyo Israel na Hamas wamewahi kupigana, mzozo ambao umevuruga eneo zima la Mashariki ya Kati na kusababisha maandamano katika sehemu mbalimbali duniani.

Makubaliano pia yataleta afueni ndani ya ukanda wa Gaza ulioharibiwa vibaya kufuatia oparesheni ya kijeshi ya Israel. Kando na uharibifu, takriban asilimia 90 ya wakaazi wa Gaza wapatao milioni 2.3 wamepoteza makaazi yao huku wengi wakikabiliwa na baa la njaa.

Waandamanaji mjini Tel Aviv wakishinikiza kuachiliwa huru kwa mateka. Picha: JACK GUEZ/AFP

Hata hivyo iwapo makubaliano yatafikiwa, hayatatekelezwa mara moja.

Mpango huo utahitaji idhini kutoka kwa baraza maalum la usalama la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na kisha baadaye baraza lake zima la mawaziri. Mabaraza yote hayo yanatawaliwa na washirika wa Netanyahu na kwa kiasi kikubwa, yanatarajiwa kuunga mkono mapendekezo yoyote yatakayowasilishwa kwao.

Hapo awali, maafisa walionyesha matumaini pia ya kufikiwa makubaliano, japo baadaye mazungumzo hayo yakaingia doa huku kila upande zikitupiana lawama.

Soma pia: Israel yakosolewa kwa kutaka kulipiga marufuku UNRWA 

Lakini tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma, kila dalili wakati huu zinaashiria kufikiwa kwa makubaliano hayo kabla ya kuapishwa kwa Rais mteule wa Marekani Donald Trump mnamo Januari 20, ambaye mjumbe wake wa Mashariki ya Kati pia amejiunga kwenye mazungumzo hayo.

Hamas imeeleza katika taarifa kwamba mazungumzo yamefikia hatua ya mwisho.

Tizama namna Wapalestina wanavyopambania mkate

01:57

This browser does not support the video element.

Wakati hayo yanaripotiwa, maelfu ya watu wamekusanyika mjini Tel Aviv kuunga mkono makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo wamekuwa wakiyahimiza kwa muda mrefu.

Mateka mmoja aliyeachiliwa kutoka Gaza Moran Stella Yanai amesema, "Hili sio suala la siasa au mikakati. Ni kuhusu utu na imani ya pamoja kwamba hakuna mtu yeyote anayepaswa kuachwa gizani."

Hata hivyo mjini Jerusalem, mamia ya watu wenye misimamo mikali waliandamana kupinga makubaliano hayo. Baadhi wakiimba nyimbo na kueleza upinzani wao kwamba, Israel haipaswi kuingia makubaliano na shetani, wakimaanisha kundi la Hamas.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW