1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yasema bado mapambano yanaendelea Gaza

21 Aprili 2022

Kiongozi wa kundi la Hamas katika ukanda wa Gaza, Ismail Haniya ametishia kuzidisha makali ya mapigano kati ya kundi hilo na Israel baada ya pande zote mbili kwa mara nyengine kurushiana makombora usiku kucha.

Israel I Gaza I Ashkelon
Picha: Amir Cohen/REUTERS

Wanamgambo hao wa Ukanda wa Gaza walirusha maroketi yaliyoulenga mpaka wa Israel Jana jioni na mapema leo alfajiri. Ving'ora vya kuashiria hali ya hatari vilisikika mara mbili Kusini mwa Israel hii ikiwa ni kulingana na jeshi la taifa hilo. Israel nayo ilijibu kwa kuyashambulia mahandaki yenye vituo vya Hamas vya kutengeneza maroketi kwa nia ya kupunguza uwezo wa wapalestina kutengeneza silaha hizo.

soma zaidi: Israel yashambulia kwa ndege za kivita Kusini mwa Gaza

Pande zote mbili zimekuwa katika mapigano makali wiki hii wakati wanajeshi wa Israel walipopambana na raia wa palestina katika eneo takatifu la Jerusalem. Watu kadhaa wamejeruhiwa katika mapambano hayo hali inayozidisha mvutano kati ya pande hizo mbili hasa wimbi la mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya wapalestina.

Machafuko hayo kwenye mpaka wa Gaza, yanaonekana kuwa mapigano makubwa zaidi tangu vita vya mwaka jana wakati wa mfungo wa Ramadhani vilivyodumu kwa siku 11 na yanakuja licha ya kuwepo juhudi za kuzuia marudio ya vita hivyo.

Israel imesema inawanyooshea kidole cha lawama Hamas kwa matukio yote inayoyaita ya kigaidi yanayoilenga ardhi ya Israel kutoka ukanda wa Gaza.

Hamas yasema inatarajia kushinda kile ilichosema ni sera ya uvamizi ya Israel

Kiongozi wa kundi la Hamas Ismail HaniyehPicha: AP

Hata hivyo kundi la Hamas kupitia kiongozi wake Ismail Haniya limesema ndio mwanzo limeanza mapambano na lina imani ya kushinda ilichokitaja kuwa ''sera ya uvamizi''.

Polisi ya Israeli imesema waandamanaji waliofunika nyuso zao walikusanyika katika msikiti wa Al Aqsa wakafunga mlango na kuanza kurusha mawe na mabomu ya petroli. Polisi hiyo iliongeza kuwa ilijaribu kuwatawanya waandamanaji hao wa kipalestina kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi. Kulingana na shirika la hilali nyekundu watu 20 walijeruhiwa na mwengine mmoja kuwa katika hali mahututi.

Eneo la msikiti wa Al Aqsa ndio kitovu cha vurugu kati ya waumini wa dini ya kiislamu na ya Kiyahudi. Msikiti huu ni eneo muhimu la tatu lililotakatifu kwa waumini wa kiislamu na  ni eneo takatifu zaidi kwa Wayahudi.

soma zaidi: Jeshi la Israel ladaiwa kutekeleza mauaji Ukingo wa Magharibi

Wapalestina pamoja na mashirika ya kutetea haki za binaadamu yamekuwa yakiishutumu Israel kutumia nguvu kupita kiasi katika kuwadhibiti wapalestina. Mitandao ya kijamii upande wa palestina imesheheni mikanda ya vidio inayoonyesha wanajeshi wa Israel wakiwashambulia wapalestina wasio na silaha wakiwemo wanawake. Hata hivyo Israel imejibu na kusema wapalestina ndio wanaochochea vurugu huku wakitoa vidio pia zinazoonesha vijana wa kipalestina wakiwarushia mawe maafisa wa polisi na kuwaweka hatarini watu walioko karibu.

Chanzo: dpa/ap

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW