1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yasema Biden anaipa Israel "Tiketi" ya kuendeleza vita

20 Agosti 2024

Hamas imelaani matamshi yaliotolewa na Rais wa Marekani Joe Biden kwamba kundi hilo la Kipalestina lilikuwa linajiondoa kwenye makubaliano ya kusitisha vita Gaza, likiyataja kuwa ya kupotosha.

Gaza Israel Krieg - Luftangriff und Geflüchtete kn Khan Yunis
Picha: Hatem Khaled/REUTERS

Hayo yanajiri wakati Rais wa Misri Abdel-Fattah Al-Sisi ameonya juu ya hatari ya kutanuka kwa mzozo huo kwa namna ambayo ni ngumu kufikirika alipokutana na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, alieko Mashariki ya Katika kushinikiza muafaka wa kusitisha vita Gaza.

Hamas imesema katika taarifa kuwa matamshi ya kupotosha ya Biden hayaakisi msimamo sahihi wa vuguvugu hilo, ambalo liko makini kufikia mapatano ya kusitisha vita, na kuyataja matamshi ya Biden, aliyoyatoa Jumanne wakati akijiandaa kuondoka Chicago baada ya kuhutubia mkutano mkuu wa chama cha Democratic, kuwa idhini ya Marekani kwa seriali ya itikadi kali ya Kizayuni kutenda uhalifu zaidi dhidi ya raia wasioweza kujilinda.

Tamko hilo la Hamas limekuja wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akiwa nchini Misri kwa mazunguzo juu ya mpango wa kusitisha vita Gaza. Blinken ambaye alikutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem siku ya Jumatatu, kabla ya kuelekea nchini Qatar, ambayo, pamoja na Misri zinaratibu majadiliano ya mapatano katika mzozo huo uliodumu kwa zaidi ya miezi 10 sasa.

Soma pia:Blinken apeleka msukumo wa mapatano Gaza Misri 

Hamas imesema matamshi ya Biden yanaakisi "upendeleo wa wazi wa Marekani" kuelelea Israel na ushiriki wa Washington katika vita vya maangamizi dhidi ya raia wasioweza kujilinda katika Ukanda wa Gaza.

Rais Joe Biden akizungumza katika siku ya kwanza ya mkutano mkuu wa chama cha Democratic mjini Chicago, Agosti 19, 2024.Picha: Mike Segar/REUTERS

Kundi hilo limesema limejitolea kutekeleza mpango ulioainishwa na Biden Mei 31, ambao alisema ulipendekezwa na Israel. Imeyataja marekebisho ya karibuni ya Marekani kwa mpango huo, kama "mapinduzi dhidi" ya mfumo wa awali, na kuituhumu Washington kukubali tu masharti ya Netanyahu.

Israel yashambulia tena shule inayohifadhi wakimbizi

Huko Gaza kwenyewe, shirika la ulinzi wa raia limesema shambulizi la Israel dhidi ya shule iliyogeuzwa hifadhi limeuawa watz wasiopungua 12, huku Israel ikisema imeshambulia kituo cha kamandi ya Hamas.

Msemaji wa shirika hilo Mahmud Bassal, ameliambia shirika la Habari la AFP kuwa wafanyakazi wao wamepata miili 12 kutoka shule hiyo, ambayo inawahifadhi maelfu ya Wapalestina.

"Ghorofa nzima au upande mzima wa shule hii umelengwa. Shule hii inahifadhi takriban watu 700 waliohamishwa ambao wamekuwa hapa tangu kuanza kwa vita hadi wakati huu. Idadi ya awali ni karibu na mashahidi kumi katika shambulio hili," alisema Bassal.

Soma pia: Blinken amsisitizia Netanyahu akubali kusitisha vita Gaza

"Kuna watu kadhaa waliofunikwa na vifusi. Wafanyakazi wa matibabu na raia wanajaribu kupata chochote kinachoweza kupatikana."

Jeshi la Israel limesema shule hiyo ililengwa kwa sababu ilihifadhi kituo cha kamandi na udhibiti cha Hamas, ambacho kilikuwa kinapanga mashambulizi dhidi ya wanajeshi wake na taifa la Israel.

Mapacha vichanga wauwawa Gaza

01:04

This browser does not support the video element.

Kisasi cha Iran dhidi ya Israel kinaweza kuchukua muda mrefu

Katika taarifa nyingine kikosi cha walinzi wa mapinduzi ya Iran kimesema mashambulizi yake ya kisasi dhidi ya Israel yanaweza kuchukuwa muda mrefu, na kuongezka kuwa Iran inaunga mkono hatua zozote zinazopelekea kumalizi vita Gaza.

Hata hivyo msemaji wa kikosi hicho Alimohammad Naini, amesema matukio ya kikanda hayana uhusiano wowote na haki yao ya kisasi dhidi ya Israel.

"Wakati upo kwa ajili yetu na muda wa kusubiri majibu haya unaweza kuwa mrefu," Naini alisema, akimaanisha uwezekano wa kulipiza kisasi dhidi ya Israel. Alisema "adui" anapaswa kusubiri majibu yaliyohesabiwa na sahihi.

Viongozi wa Iran walikuwa wakitathmini mazingira na majibu ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu huenda yasiwe marudio ya operesheni za awali, aliongeza, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW