1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Hamas yasema makubaliano ya kusitisha vita Gaza yanakaribia

21 Novemba 2023

Mapigano yameendelea kwenye Ukanda wa Gaza leo Jumanne lakini pamejitokeza mwanga wa matumaini baada ya kiongozi wa kundi la Hamas kusema makubaliano ya kusitisha vita kati yake na Israel yananukia.

Majengo yaliyoharibiwa Ukanda wa Gaza
Ukanda wa GazaPicha: Leo Correa/AP Photo/picture alliance

Hayo yametangazwa katika wakati idadi ya watu waliouwawa huko Gaza imefikia 13,300, takwimu hizo ikiwa ni kwa mujibu wa wizara ya afya ya kundi la Hamas.

Kiongozi wa kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza Ismail Haniyeh ametoa habari za matumaini mapema hii leo akisema wanaelekea kupata makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel yaliyodumu kwa muda wa wiki sita.

Ofisi yake imetoa ujumbe mfupi tu uliotumwa kwa mashirika kadhaa ya habari ukisema, "Tumekaribia kupata mkataba wa kusitisha mapigano." 

Taarifa yake imeleta vilevile matumaini kwamba mateka kadhaa wanaoshikiliwa na kundi la Hamas tangu shambulizi la Okotba 7 ndani ya ardhi ya Israel huenda wataachiwa huru.

Suala la kuachiwa mateka limekuwa moja ya masharti makuu ya serikali ya Israel ili alau itafakari kusitisha kampeni yake ya kijeshi dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Kampeni hiyo ilianzishwa saa chache tu baada ya wapiganaji wa Hamas kuingia Israel na kufanya shambulizi ambalo mamlaka mjini Tel Aviv zinasema liliwauwa watu 1,200.

Ni wachache tu kati ya mamia ya mateka waliochukuliwa na wapiganaji wa Hamas ndiyo wameachiwa huru. Israel inakadiria wale waliobakia mikononi mwa kundi hilo wanapindukia 240 ikiwemo watoto pamoja na wazee.

Mateka kuachiwa kwa makubaliano ya kuachiwa pia Wapalestina 

Kiongozi wa kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza Ismail HaniyehPicha: Hatem Moussa/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Taarifa za uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita zimetolewa vile vile na duru kadhaa za habari ambazo hazikutajwa lakini ni kutoka ndani ya kundi la Hamas na lile la Islamic Jihad lililoshiriki shambulizi la Oktoba 7.

Inaarifiwa miongoni mwa makubaliano ni kusitishwa mapigano kwa muda wa siku 5 hususani operesheni ya ardhini ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza na kupunguza hujuma za ndege za kivita za Israel mashariki mwa ukanda huo.

Chini ya mkataba huo, mateka kati ya 50 hadi 100 wanaojumuisha raia wa Israel na wale wa kigeni pekee ndiyo wataachiwa.

Hakuna mateka wa kijeshi atakayeachiwa huru. Upande wa Hamas unataraji kiasi Wapalestina 300 wanaoshikiliwa kwenye jela za Israel wataachiwa ikwiemo watoto na wanawake.

Kadhalika inatarajiwa iwapo masharti ya kila upande yataridhiwa, makubaliano yatakayopatikana yatawezesha pia kuruhusiwa malori 300 ya msaada kila siku kuingia Ukanda wa Gaza.

Biden aelezea matumaini wakati Israel yaendelea kuishambulia Gaza 

Mvua kubwa iliyonyesha Ukanda wa Gaza mnamo Novemba 19, iliongeza kishindo kwa wakaazi wa eneo hilo.Picha: Fatima Shbair/AP/picture alliance

Hapo jana Jumatatu, rais Joe Biden wa Marekani naye alidokeza juu ya kufikiwa mkataba hivi karibuni. Kwa sehemu kubwa mazungumzo ya kupata makubaliano hayo yanaratibiwa na Qatar, taifa la ghuba lenye mahusiano ya karibu na kundi la Hamas lakini masikilizano na watawala nchini Israel.

Ndani ya Gaza kwenyewe hamkani bado si shwari. Mashambulizi ya Israel yameendelea, huku vikosi vyake vikitanua hujuma kote kaskazini mwa ukanda huo.

Maafisa wa wizara ya afya inayoongozwa na Hamas imesema Israel imewauwa watu 12 baada ya kuilenga kwa makombora hospitali iliyojengwa kwa hisani na Indonesia. Msemaji wa wizara hiyo Ashraf al-Qudra amesema "Jeshi la Israel limeizingira hospitali" hiyo.

Israel imekuwa ikifanya operesheni yake ndani ya hospitali za Ukanda wa Gaza kwa hoja kwamba kundi la Hamas linatumia majengo ya vituo vya matibabu kuendesha shughuli zake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW