1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamburg yajiondoa katika eneo hatari

8 Desemba 2014

SV Hamburg iliizaba Mainz magoli mawili kwa moja hapo jana na kuondoka katika eneo hatari la kushushwa daraja. Ilikuwa wikendi nzuri pia kwa Augsburg ambao sasa wako katika nafasi ya tatu ya Bundesliga

Bundesliga - 14. Spieltag: Hamburger SV - FSV Mainz 05
Picha: picture-alliance/dpa/M. Christians

Bao la kwanza la Hamburg lilifungwa na beki Mbrazil huku nahodha Rafael van der Vaart akifunga la pili kwa njia ya penalty. Shinji Okazaki aliwafungia Mainz goli la kufutia machozi.

Hamburg ilisonga hadi nafasi ya 13 kutoka nafasi ya pili ya mkia ya 17 na kuziruka timu za Bremen, Freiburg, Hertha Berlin na Borussia Dortmund. Hamburg wana points 15 baada ya kushinda mchuano wa tatu wa nyumbani mfululizo.

Nambari 11 Mainz hawajashinda katika mechi sita na wako juu ya Hamburg na faida ya goli point moja pekee. Huyu hapa nahodha wa Hamburg Rafael van der Vaart "Ulikuwa mchuano mgumu kwetu. Tukiwa nyumbani, tunastahili kushinda, bila shaka shinikizo kawaida huwepo. Lakini tumefanya vyema, hata kama haukuwa mchezo mzuri wa kandanda. Tulijiamini na pia kuna wakati bahati ilituendea upande wetu lakini nadhani tulistahili kushinda. Ilikuwa vigumu hasa wakati ilikuwa bado 2-1 zikisalia dakika tatu mchezo kuisha lakini hatimaye tuna points tatu na hilo ndio muhimu".

Augsburg wamewashangaza wengi kwa kusajili matokeo bora kufikia sasa msimu huuPicha: Daniel Kopatsch/Bongarts/Getty Images

VfB Stuttgart wanashikilia mkia na points 12. Katika mechi ya pili jana Alexander Meier aliifungia Eintracht Frankfurt magoli mawili wakati ikiwabamiza Werder Bremen magoli matano kwa mawili.

Siku ya Jumamosi, Bayern Munich waliendeleza rekodi yao ya kutoshindwa mechi yoyote katika Bundesliga ili kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi na pengo la points saba dhidi ya wapinzani wao wa karibu Wolfsburg. Hii ni baada ya Bayern kuwashinda Bayer Leverkusen bao moja kwa sifuri ambapo Franck Ribery aliwafungia miamba hao wa Bavaria goli lake la 100. Kichapo hicho kina maana vijana hao wa kocha Roger Schmidt Leverkusen, wameteremka hadi katika nafasi ya nne. Simon Rolfes, ni nahodha wa Leverkusen "Nadhani tulicheza vyema kwa kipindi kirefu. Tulipata nafasi kadhaa nzuri hasa katika kipindi cha kwanza ambazo tungeweza kuzitumia kwa sababu ni wazi kuwa ukiwa hapa hauwezi kupata nafasi nyingi. Kisha kwa bahati mbaya tukafungwa moja bila muda mfupi baada ya kipindi cha mapumziko, lakini hatukuweza kujipenyeza vyema katika nafasi za hatari".

Wolfsburg ilishinda mchuano wake wa ugenini mabao matatu kwa moja dhidi ya mahasimu wao wa jimbo la Lower Saxony Hanover 96. Kocha wa Wolfsburg Dieter Hecking anadai kuwa wao siyo wawindaji wa Bayern, kama wasemavyo waandishi wa habari Ujerumani "Tulijiweka sawa kabisa katika mchezo huo kwa kupata goli la mapema, lakini tukapunguza kasi na kuiruhusu HANOVER kujiimarisha mchezoni. Tulikabiliana kwa asilimia 50 kwa 50. Ni katika kipindi cha pili pekee ambapo nilikuwa na hisia kuwa kama tungeongeza kasi katika mchezo wetu, nafasi zetu zingeanza kupatikana na hilo likafanyika. Nadhani tulipoongoza mbili moja, mtu anaweza kuona tulikuwa imara na kisha goli la tatu likapatikana kutokana na sababu hiyo".

Eric Maxim Choupo-Moting (Kulia) alitikisa wavu mara tatu katika ushindi wao dhidi ya StuttgartPicha: Patrik Stollarz/AFP/Getty Images

Katika matokeo mengine, timu yake Roberto Di Matteo, Schalke iliibambua Stuttgart magoli manne kwa bila. Matokeo hayo yameisogeza timu hiyo katika nafasi ya nne ya ligi wakati Stuttgart yake Huub Stevens ikishikilia mkia.

Nambari tano Borussia Moenchengladbach ilipata ushindi wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Hertha Berlin, ambao wameanguka katika nafasi ya 15.

Augsburg imejizatiti na kusonga katika nafasi ya tatu, kwa mara ya kwanza katika historia yao kufiatia ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Cologne, na kocha Markus Weinzierl ameridhika na kazi waliyoifanya kufikia sasa. "Ningefurahia kama tungepata pointi moja, lakini tulijiamini hadi mwisho. Ni wazi leo tuna furaha kubwa kutokana na goli la dakika za mwisho za mchezo. Katika kipindi cha pili tulikuwa timu bora na tulishambulia zaidi na hivyo tulistahili ushindi, hata ingawa ulipatikana katika dakika ya 89". Freiburg ilitoka sare ya goli moja ka moja na Paderborn. Dortmund ilishusha pumzi baada ya kupata ushindi wa goli moja kwa sifuri dhidi ya Hoffenheim.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW