Hamburg yawania kujiokoa kushuka daraja
22 Februari 2014Ni lazima kubakia katika daraja la kwanza, ndivyo viongozi wa Hamburg SV wanavyojaribu kufanya katika klabu hiyo kongwe katika bundesliga.
Hata hivyo kubakia katika daraja hiyo ya juu ni jambo la kutia shaka kidogo, baada ya wiki ya mtafaruku katika nyanja ya michezo, pamoja na uongozi pia.
Kocha mpya wa klabu hiyo ambayo inashika nafasi ya pili kutoka mkiani mwa ligi ya Ujerumani Bundesliga Mirko Slomka anataka kuitoa klabu hiyo kongwe kutoka katika nafasi hiyo.
Hata hivyo kuna faida inayoielekea Hamburg , kwasababu mtafaruku unawakabili baadhi ya washindani wake pia katika mchezo huu wa 22 katika Bundesliga.
Mchezo wa kuamua hatima
Ni mchezo wa 22 wenye mtafaruku. Kocha wa Borussia Dortmund Jurgen Klopp timu ambayo inapambana na Hamburg leo jioni , amedokeza kuwa na hapa namnukuu ; "Ilibidi kufuta utaratibu wetu wote wa matayarisho.
Hamburg imeongeza maradufu mazowezi yao ya matayarisho dhidi yetu, na kujaribu mbinu mbali mbali tofauti ", ameongeza Klopp.
Mchezaji wa kati wa Borussia Dortmund ameongeza kuwa , anashauku kubwa kuona jinsi timu hiyo ya mjini Hamburg itakavyobadilika. Hata hivyo amesema kuwa hatarajii mchezo wa Borussia kubadilika.
Timu nyingine ambayo imo katika mbinyo mkubwa ni VFB Stuttgart. Kama ilivyo Hamburg , Stuttgart ni moja kati ya vigogo vya soka la Ujerumani na inakabiliwa na hali ya kuporomoka baada ya kushindwa mara sita mfululizo na inataka kujitoa katika eneo hatari la kushuka daraja.
Timu hiyo ya mjini Stuttgart inakwaana na Hertha BSC Berlin na itamkosa mchezaji wake muhimu na nahodha wa timu hiyo Christian Gentner.
Borussia Moenchengladbach iko nyumbani ikiwasubiri Hoffenheim , Freiburg inaikaribisha nyumbani FC Ausburg , wakati VFL Wolfsburg ina miadi na Bayer Leverkusen, timu hizo kila moja ikiwania matarajio tofauti.
Leverkusen ambayo iko katika nafasi ya pili ikiifukuzia Bayern Munich licha ya tofauti ya points 16 kati yao ,inataka kuendelea kubakia katika nafasi ya pili , wakati Wolfsburg iliyoko katika nafasi ya tano ikiwa na points 39 inawania kuchupa hadi nafasi ya kucheza katika Champions League.
Michezo mingine ni hapo Jumapili ambapo Eintrach Frankfurt itakapoikaribisha Werder Bremen na Bayern Munich ni wageni mara hii wa Hannover 96.
Premier League
Huko nchini Uingereza Manchester City itajaribu kurejesha matumaini yake katika kunyakua taji la Premier League dhidi ya Stoke City leo jioni baada ya kuangukia pua katika mchezo wa katikati ya wiki wa Champions League dhidi ya Barcelona.
Wakati huo huo kocha wa Chelsea Jose Mourinho atahitaji kikosi chake kuonesha mchezo mwingine wa matumaini ili kujaribu kuimarisha nafasi yao kileleni mwa Premier League dhidi ya Everton leo jioni.
Michezo mingine ni kati ya Arsenal London ikikumbana na Sunderland, Cardiff City dhidi ya Hull City , Cristal Palace iko nyumbani dhidi ya Manchester United na West Bromwich Albion inakwaana na West Ham United.
Nchini Uhispania Real Madrid iko nyumbani leo jioni ikiikaribisha Elche, wakati Barcelona inayoongoza ligi hiyo iko ugenini ikikabana koo na Real Sociedad.
Mwandishi. Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman