Hamdok arudishwa tena madarakani Sudan
21 Novemba 2021Jeshi la Sudan limemrudisha madarakani waziri mkuu Abdalla Hamdok leo Jumapili na kutangaza kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa waliokamatwa baada ya wiki kadhaa za machafuko yaliyochochewa na mapinduzi.
Chini ya makubaliano yaliyosainiwa leo pamoja na jenerali AbdelFatah al Burhani,Hamdok ataiongoza serikali ya kiraia ya wataalamu katika kipindi cha mpito.
Waziri mkuu huyo kwa upande wake amesema amefikia makubaliano hayo ili kumaliza umwagikaji damu nchini Sudan. Bwana Hamdok amenukuliwa akisema-
''Damu ya Wasudan inathamani,tusitishe umwagikaji damu na tuziongoze nguvu za vijana katika ujenzi na maendeleo'' Mwisho wa kumnukuu. Lakini muungano wa kiraia uliogawana madaraka na jeshi kwenye serikali iliyokuwepo umesema unapinga mazungumzo yoyote na jeshi na wametaka maandamano zaidi yanedelee hii leo.
Makubaliano hayo ya kufungua ukurasa mpya wa kisiasa nchini Sudan yanakuja baada ya kufanyika mazungumzo marefu ya kina baina ya viongozi wa kijeshi waliofanya mapinduzi na wawakilishi wa kiraia.
Ikimbukwe kwamba bwana Hamdok aliteuliwa waziri mkuu kuiongoza serikali ya mpito mnamo mwaka 2019 baada ya maandamano makubwa sana yaliyomuondowa madarakani kiongozi wa zamani aliyeitawala nchini hiyo kwa miongo kadhaa, Dikteta Omar al Bashir.
Serikali ya waziri mkuu Hamdok kimsingi ilipewa jukumu la kuandaa uchaguzi ujao ambao kwahakika ungelifanya jeshi kulazimika kupisha utawala kamili wa serikali ya kiraia. Wakati wa kipindi cha mpito Sudan ilikuwa ikiongozwa na baraza huru la utawala ambalo liliwajumuisha pia wanajeshi na viongozi wa kiraia.
Makubaliano hayo ya utawala wa kugawana madaraka yalionekana kuvunjwa mnamo mwezi uliopita wa Oktoba pale jenerali Abdel Fattah al Burhani alipoamua kuivunja serikali na kumuweka waziri mkuu Hamdok kwenye kifungo cha nyumbani na kutangaza hali ya hatari.
Lakini Wasudan waliingia tena mitaani na kufanya maandamano ya kila uchao yaliyoshuhudia vurugu na watu 15 kuuwawa katika duru ya hivi karibuni ya maandamano hayo.Ni baada ya wanajeshi kuwashambulia kwa risasi za moto waandamanaji.