1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamkani bado si shwari Ufaransa kufuatia kifo cha Nahel

1 Julai 2023

Maelfu ya waandamanaji vijana wamepambana na polisi na kupora maduka kwenye miji mbalimbali nchini Ufaransa inayokumbwa na ghasia zilizotokana na kifo cha kijana wa maika 17 aliyepigwa risasi na polisi.

Ghasia zimehusisha uchomaji wa mali
Maelfu ya polisi wametajwa Ufaransa kupambana na ghasiaPicha: Jean-Francois Badias/AP/picture alliance

Ghasia hizo za usiku wa nne mfululizo zimeongeza shinikizo kwa utawala wa rais Emmanuel Macron hata baada ya kuwarai wazazi kuwazuia watoto wao kuingia mitaani na kuilaumu mitandao ya kijamii kwa kuchochea vurugu.

Ijapokuwa usiku wa kuamkia Jumamosi, hali imeonekana imetengamaa kidogo ikilinganishwa na siku tatu zilizotangulia, machafuko bado yameigubika miji kadhaa ya Ufaransa.

Wazima moto kwenye kitongoji cha mji mkuu Paris cha Nanterre, eneo ambako ndiyo afisa wa polisi alifyetua risasi na kumuua kijana huyo aliyetambulishwa kwa jina la Nahel, walipambana kuzima mioto iliyowashwa na waandamanaji. Kwa sehemu kubwa magari yaliyochomwa yaliteketea.

Kwenye kitongoji jirani cha Colombes, waandamanaji waipindua madebe ya taka na kuzikusanya kuweka kizuizi kwa polisi kuwafikia.

Kwenye mji wa mwambo wa Marseille, maafisa wa polisi wamewakamata karibu watu 90 kutoka makundi ya waandamanaji ambao wamechoma magari na kuvunja madirisha ya maduka kukwapua vilivyomo.

Waporaji kwenye mji huo walivamia duka moja la kuuza silaha na kutoroka nazo, na mwanaume mmoja alikamatwa baadae akiwa amekwapua bunduki ya kuwindia.

Rais Macron achagua ubavu wa maafisa wa polisi badala ya hali ya hatari 

Mapambano ni makali kati ya polisi na waandamanajiPicha: Jean-Francois Badias/AP Photo/picture alliance

Majengo na maduka ya biashara yamehujumiwa kwa mara nyingine kwenye mji wa mashariki wa Lyon, eneo ambalo karibu theluthi ya watu 30 waliokamatwa wanatuhumiwa kwa wizi.

Katikati ya mzozo unaozidi makali ambao umeshuhudia mamia ya watu wakikamatwa na maelfu wa polisi wakitawanywa, rais Emmanuel Macron bado amejizuia kutangaza hali ya hatari kwa ngazi ya taifa, chaguo ambalo lilitumika kukabiliana na hali kama hiyo mwaka 2005.

Badala yake, serikali anayoiongoza imeongeza juhudi za kiusalama kujaribu kupambana na vurumai hiyo. Idadi ya polisi imeongezwa na kufikia 45,000 .

Wengine wameitwa kutoka likizo. Inaarifiwa watu 917 wamekamatwa siku ya Alhamisi pekee na wengi ni vijana walio na angalau na umri wa miaka 17. Wizara ya mambo ya ndani imesema maafisa 300 wamejeruhiwa.

Kifo cha Nahel kimetonesha kidonda cha malalamiko dhidi ya polisi 

Vurugu hizo za maelfu ya watu zinasemwa ni kwa lengo kulaani kifo cha kijana mmoja mwenye umri wa miaka 17 aliyepigwa risasi na polisi siku ya Jumanne.

Uharibifu ni mkubwa kwenye ghasia zilizoshuhudiwa Ufaransa Picha: Laurent Cipriani/AP Photo/picture alliance

Kifo cha kijana huyo kimetonesha kidonda cha hasira miongoni mwa wafaransa juu ya jinsi polisi ya nchi hiyo inavyofanya kazi na madai ya ubaguzi unaozilenga jamii za wasio wazungu.

Inaarifiwa siku ya tukio, kijana aliyeuwawa alisimamishwa na polisi kwa makosa ya kuendesha gari kwa mwendo mkubwa. Walimtaka kuzima chombo hicho lakini  ghafla kijana huyo aliondoa gari lake haraka na hapo ndipo afisa anayechunguzwa alifyetua risasi iliyomua.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameutaja mkasa huo kuwa "usiosameheka" lakini amewataka waandamanaji kusitisha vurugu akisema matendo yao "hayakubaliki".

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW