1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haniyeh: Vifo vya wannagu Israel inajidanganya

11 Aprili 2024

Kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh amesisitiza kwamba vifo vya watoto wake watatu katika shambulio la anga la Israel hakutaathiri mazungumzo ya usitishwaji vita vya Gaza na kwamaba Israel inajidanganya

Iran /Teheran |  Ismail Haniyey
Ismail Haniyeh, Kiongozi wa kundi la HamasPicha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh amesisitiza kwamba vifo vya watoto wake watatu katika shambulio la anga la Israel hakutaathiri mazungumzo ya usitishwaji vita vya Gaza, wakati hayo yakijiri, Marekani imeihakikishia Israel kuwa itasimama upande wake dhidi ya vitisho vyovyote vinavyotolewa na Iran.

Israel imethibitisha vifo vya wanawe Haniyeh ambavyo vinajiri wakati mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka wa Israel yakiendelea bila dalili yeyote ya mafanikio.

Soma zaidi. Israel yakabiliwa na shinikizo kubwa kuhusu vita vyake Gaza

Akizungumza na shirika la utangazaji la Qatar la Al Jazeera,Ismail Haniyeh, kiongozi wa kundi la Hamas amesema shambulio hilo liliouwaua pia wajukuu wake wanne lilikuwa ni jaribio la kubadilisha msimamo wa mazungumzo wa Hamas jambo ambalo anasema Israel inajidanganya.

Ismael Haniyeh, Kiongozi wa kundi la Hammas amesema vifo vya watoto wake havitoathiri mazungumzo ya HamasPicha: Vahid Salemi/AP/dpa/picture alliance

Wakati wa mazishi ya watoto wa kiongozi huyo, mmoja wa ndugu wa Ismail Haniyeh ambaye hakutajwa jina lake amekaririwa akisema kwamba ushindi dhidi ya mapambano yao na Israel ni lazima.

Blinken: Marekani inasimama na Israel

Kwa upande mwingine, Marekani ambayo ni mshirika mkuu wa Israel imekuwa ikizidisha shinikizo kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kukubaliana na mapatano, kuruhusu misaada kuingia katika ukanda wa Gaza na kuachana na mpango wake wa kuushambulia mji wa kusini wa Rafah.

Ingawa mapema leo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, katika mazugumzo yake ya simu na Waziri wa Ulinzi wa Israeli Yoav Gallant ameweka wazi kuwa Marekani itasimama na Israel dhidi ya vitisho vyovyote vinavyotolewa na Iran inayoliunga mkono kundi la Hamas.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema kwamba Marekani itasimama na Israel dhidi ya kitisho chcochotePicha: Johanna Geron/Pool Reuters/AP Photo/dpa

Soma zaidi. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lashindwa kupitisha azimio la kusitisha mapigano Gaza

Yoav Galant ameongeza pia kuwa Israel imefungua njia mpya ya kupitisha misaada kwa Wapalestina katika eneo la kaskazini mwa Gaza la bandari ya Ashdodi.

Hata hivyo, wakati jitihada hizo zikiendelea bado hali mashariki ya kati ipo mashakani. Shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa limesema kuwa lilisitisha shughuli zake za ndege kwenda Tehran kutokana na hali ilivyo Mashariki ya Kati ambayo iko katika tahadhari kutokana na shambulizi linaloshukiwa kufanywa na Israel katika ubalozi wa Iran nchini Syria. 

Shirika la ndege la Ujerumani la Lufthansa limesema lilisimamisha safari hizo kuanzia Aprili 6 hadi leo tarehe 11Picha: Frank Hoermann/SVEN SIMON/picture alliance

Nchi katika eneo la Mashariki ya Kati zimekuwa katika tahadhari tangu Aprili Mosi na zimekuwa zikijiandaa kwa uwezekano wa shambulizi la Iran.

Shirika la Lufthansa limesema lilisimamisha safari hizo kuanzia Aprili 6 hadi leo tarehe 11.