HANOI: Korea ya Kaskazini yahimizwa kuachulia mbali mradi wa kinuklia
19 Novemba 2006Mkutano wa nchi 21 zinazoshirikiana kiuchumi katika eneo la Asia na Pacifik-APEC umetoa mwito kwa Korea ya Kaskazini kusitisha mpango wake wa kutengeneza silaha za kinuklia.Katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa mkutano wa kilele wa APEC nchini Vietnam,viongozi wa nchi na serikali wameeleza wasi wasi wao kuhusu jaribio la kinuklia lililofanywa na Korea ya Kaskazini mwezi wa Oktoba.Serikali ya kikomunisti ya Pyongyang, imehimizwa kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa na kurejea kwenye meza ya majadiliano.Mbali na mada ya kinuklia ya Korea ya Kaskazini,mkutano wa Hanoi hasa ulishughulikia masuala ya kiuchumi. Madola ya APEC,yamesisitiza kwamba majadiliano mapya yanapaswa kufanywa kuhusika na suala la kupunguza ruzuku.Nchi hizo vile vile zimeamua kushirikiana zaidi kupiga vita ulaji rushwa.