Hanover, Stuttgart zaondoka katika eneo hatari
19 Oktoba 2015Hanover ilipata ushindi wa moja sifuri dhidi ya Cologne isipokuwa picha za video zilionyesha kuwa kiungo Leon Andreasen alifuga bao hilo kwa kutumia mkono. Na ni bao ambalo lilimwacha kocha wa Cologne Peter Stoeger na hasira "Nilimwambia Andreasen hapaswi kuomba radhi. Kutokana na mambo yalivyokuwa siyo kosa lake. hiyo ni kazi ya refarii na wasaidizi wake. Kuna mengi hapa ambayo yangeweza kuonekana. Kama haukuona goli la mkono basi angalau ungeona kosa la hapo kabla. Na kama haukuona vyote viwili, basi haukufanya maamuzi mazuri".
Hanover sasa hawajashindwa katika michuano yao mitatu iliyopita na wamepanda hadi nafasi ya 14, huku nao Cologne wakianguka hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi.
Stuttgart ilipanda hadi nafasi ya 15 kutoka 18 baada ya ushindi wao wa moja sifuri dhidi ya Ingolstadt, lakini picha za video zilionyesha kuwa mfungaji goli Daniel Didavi alikuwa ameotea. Hata hivyo hilo halikumjalisha kocha wa Stuttgart Alexander Zorniger
Siku ya Jumamosi, Bayern Munich ilikuwa timu ya kwanza kushinda mechi zake zote tisa za mwanzo katika Bundesliga baada ya goli la Thomas Müller kuwapa vijana hao wa Pep Guardiola ushindi wa moja bila dhidi ya Werder Bremen. Bayern sasa wanaongoza kileleni na pengo la pointi saba dhidi ya wapinzani wao wa karibu Borussia Dortmund, waliopata ushindi wa mbili sifuri dhidi ya Mainz.
Wolfsburg ilisonga hadi nafasi ya nne baada ya kupata ushindi wa nne mbili dhidi ya Hoffenheim katika uwanja wa Volkswagen Arena. Schalke 04 wanashikilia nafasi ya tatu, pointi moja nyuma ya Borussia Dortmund, baada ya vijana hao wa samawati kuwanyamazisha Hertha Berlin magoli mawili kwa moja.
Borussia Moenchengladbach waliendelea kujiimarisha chini ya mkufunzi mpya Andre Schubert kwa kuwasambaratisha Eintracht Frankfurt mabao matano kwa moja. Bayer Leverkusen walitoka sare ya sifuri sifuri na Hamburg wakati nao Darmstadt wakiendelea kuwa na maisha mazuri kwenye Bundesliga kwa kuwashinda Augsburg mbili sifuri.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu