Harakati za kidiplomasia juu ya mzozo wa Libya
12 Julai 2011Kwa upande mwengine, Ufaransa imesema kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, yuko tayari kuacha madaraka. Kwa mujibu wa wajumbe hiyo ni ishara ya mwishoni kabisa inayoonesha kwamba mawasiliano yanafanyika baina ya kiongozi huyo wa Libya na wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO kutafuta njia za kujikwamua na mzozo huo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Alain Juppe, amesema wajumbe kutoka kwa Gaddafi wanawaambia kwamba kiongozi huyo yuko tayari kuondoka, na wajumbe hao wanataka jambo hilo lizungumziwe. Bwana Juppe alisema suali sio tena kama Gaddafi ataondoka, lakini ni lini na vipi.
Naye waziri mkuu wa Libya, Baghdadi al-Mahmudi, ameliambia gazeti la Ufaransa, Le Figaro, katika mahojiano yaliofanywa Tripoli hii leo, kwamba utawala wake ulio vitani uko tayari kuanza kufanya mazungumzo na Ufaransa na waasi wa Libya, bila ya kuweka masharti na bila ya kujiingiza Gaddafi katika mashauriano hayo. Alisema Gaddafi hatoshiriki katika mazungumzo hayo, na kila kitu kizungumziwe. Waziri mkuu huyo wa kutoka Tripoli alisema wao wako tayari kufanya mashauriano bila ya kuweka masharti, wanataka tu yasitishwe mashambulio ya NATO ili yafanyike mazungumzo katika hali ya utulivu. Alisema wao hawawezi kuzungumza wakati mabomu yanatupwa.
Kwa upande wake, Mahmud Shammam, msemaji wa Baraza la mpito la taifa huko Libya, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanamapinduzi watayajibu tu mapendekezo yalio thabiti, ambayo ni pamoja na kuondoka madarakani Gaddafi na watoto wake. Alisema mshirika wa Gaddafi, Beshir Saleh, amewasiliana na Ufaransa kupendekeza kwamba Gaddafi aondoke madarakani, lakini abakie Libya chini ya ulinzi wa kimataifa. Lakini mtoto wa Gaddafi mwenye usahwsihi mkubwa, Seif al-Islam, amelipinga wazo hilo.
Jana rais Barack Obama wa Marekani alimwambai mwenzake wa Urusi, Dmitry Medvedev, kwamba nchi yake itaunga mkono juhudi za Urusi za kuutanzuwa mzozo wa Libya, pindi Gaddafi atakubali kuwachia madaraka.
Na Uturuki imezialika China na Urusi zijiunge kwa mara ya kwanza katika mazungumzo juu ya Libya ambayo yataanza wiki hii huko Istanbul. Nchi hizo zimealikwa kama wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Nayo Uswisi imetangaza itampeleka mwanadiplomasia katika mji wa Benghazi uanoshikiliwa na waasi huko Libya afungue ofisi kwa lengo la kuimarisha maingiliano na Baraza la mpito la taifa huko Libya.
Hadi sasa madola ya NATO yamejihusisha zaidi na kufanya mashambulio ya kutokea angani na kuwaunga mkono waasi wanaojaribu kumpinduwa kutoka madarakani Gaddafi. Lakini ilivokuwa imedumu sasa miezi mitano ya uasi na hakuna alama ya kupatikana upenu, uzito sasa unabadilishwa na kuwekwa katika kutafuta suluhiso la kisiasa. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Alain Juppe alisema hivi sasa kila mtu anawasiliana na kila mtu, utawala wa Libya unapeleka wajumbe kila pahala, hadi Uturuki, New York na Paris. Hata hivyo, alishikilia kwamba hayo ni mawasiliano, lakini sio mashauriano halisi kwa wakati huu.
Bado hauijulikani kwa umbali gani zinaaminika hizo habari zilitolewa na wajumbe kutoka kwa Gaddafi, na waangalizi wengi wa mambo wanaonya kwamba iko haja ya kuwa na tahadhari kuchukuliwa kila kitu kinachotoka kwa serekali ya Libya kuwa ni kweli. Kwa mfano, mwezi April, maafisa wa Libya walisema walikuwa wanatayarisha katiba mpya na kutaka kuleta marekebisho makubwa ya kisiasa, lakini maelezo yalikuwa yao sio wazi, na hakujatajwa jmadaraka gani atakayokuwa nayo Gaddafi.
Makombora yaliofyetuliwa na majeshi yalio ttifu kwa Gaddafi jana yaliwauwa wapiganaji waasi wanane na kuwajeruhi 25 katika mwambao wa Bahari ya Mediterranean, karibu kilomita 160 mashariki ya Tripoli. Hayo yalitajwa na wafanya kazi wa hospitali katika mji wa karibu wa Misrata
Waziri wa mambo ya kigeni wa Italy, ambaye hivi sasa anatembelea nchi ilio jirani na Libya, yaani Algeria, Franco Frattini, amesema wao wana hakika kwamba mzozo wa Libya unahitaji ufumbuzi wa kisiasa kwa kusimamisha mapigano, Gaddafi ambaye amepoteza uhalali wote aondoke kutoka jukwaa la kisiasa, na kuanzishwe mchakao wa kidimokrasia utakaowaiingiza Walibya wote. Italy, mwanachama wa NATO, imetoa vituo ambavyo vinatumiwa na ndege zote za kijeshi za wanachama wa NATO zinazotumika kuishambulia Libya. Wiki iliopita waziri mkuu wa Italy, Silvio Berlusconi, alifichuwa kuweko nyufa katika muungano huo wa NATO kwa kusema yeye alipinga Libya kushambuliwa kwa mabomu. Naye waziri wa ulinzi wa Marekani, Leon Panetta, amesema baadhi ya nchi za NATO zinazofanya operesheni huko Libya zinaweza karibuni zikaona uwezo wao wa kiufundi kuendelea na operesheni hiyo umechoka. Hii ni alama nyingine ya mgawayniko ndani ya NATO.
Mwandishi:Othman Miraji/rtr
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman